• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 11:05 AM
Spurs roho juu ikiwaendea Dortmund kwa gozi kali UEFA

Spurs roho juu ikiwaendea Dortmund kwa gozi kali UEFA

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

TOTTENHAM HOTSPUR watashuka leo Jumanne dimbani kuvaana na Borussia Dortmund wakiwa na wingi wa matumaini ya kutinga robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Hii ni baada ya kusajili ushindi wa 3-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza uliowakutanisha ugani Wembley katika hatua ya 16-bora ya kipute hicho.

Kingine kinachotazamiwa kuwa kiini cha hamasa ya Tottenham ni wingi wa visa vya majeraha ambavyo kwa sasa vinatishia kulemaza pakubwa safu ya nyuma ya Dortmund.

Tangu wazidiwe maarifa uwanjani Wembley, makali ya Dortmund ambao kwa sasa wananolewa na kocha Lucien Favre yameshuka pakubwa.

Miamba hao wa soka ya Ujerumani wamesajili sare moja dhidi ya wanyonge Nurnberg katika mchuano wa Bundesliga, wakavuna ushindi wa 3-2 dhidi ya Bayer Leverkusen mbele ya mashabiki wao wa nyumbani na kupoteza dhidi ya Augsburg waliowapepeta 2-1 mwishoni mwa wiki jana.

Matokeo ya Dortmund dhidi ya Augsburg yaliwaweka vijana hao wa Favre katika hatari ya kupitwa na Bayern Munich ambao kwa upande wao waliwapepeta Borussia Monchengladbach 5-1 ugenini.

Ubora wa mabao

Cha pekee ambacho kwa sasa kinawaweka Dortmund mbele ya Bayern katika jedwali la Bundesliga ni pengo la mabao mawili zaidi yanayojivuniwa na kikosi hicho cha Favre. Dortmund na Bayern wana alama 54 kila mmoja.

Hali haijawa tofauti pia kwa upande wa Tottenham katika soka ya Uingereza. Kikosi hicho cha kocha Mauricio Pochettino kimejizolea alama moja pekee ligini tangu walipowacharaza Dortmund.

Baada ya matumaini ya kunyanyua ufalme wa Ligi Kuu ya EPL kudidimia zaidi, Pochettino amewataka sasa vijana wake kuyaelekeza macho kwa kampeni za UEFA na kupiga hatua zaidi katika kipute hicho.

Kiu ya kuyaendea mabao ya mapema dhidi ya Tottenham ni jambo ambalo litavujisha zaidi safu ya nyuma ya Dortmund na hivyo kuwapa wavamizi Son Hueng-Min, Christian Eriksen na Harry Kane nafasi za kuwafungia waajiri wao mabao zaidi.

Iwapo Tottenham watatanguliwa kuwafunga Dortmund mbele ya mashabiki wao wa nyumbani ugani Signal Iduna Park, basi wenyeji watalazimika kufunga magoli matano zaidi ili kuweka hai tumaini finyu la kufuzu kwa hatua ya nane-bora.

Tottenham hawajasajili ushindi wowote wa ugenini katika UEFA tangu walipowakomoa Dortmund mnamo 2017. Tatu kati ya mechi zao nne zilizopita ugenini zilimalizika kwa sare huku Inter Milan wakiwachabanga katika mchuano wa makundi msimu huu.

Kukutana

Hadi kufikia sasa, Tottenham na Dortmund wamekutana mara tano. Ingawa Dortmund walishinda mechi zote mbili za raundi ya 16-bora katika Ligi ya Uropa mnamo 2016, Tottenham waliibuka na ushindi katika mechi zote tatu katika UEFA.
Baada ya kuwapepeta Dortmund 3-1 mnamo Septemba 2017, Tottenham walisajili ushindi wa 2-1 ugenini mnamo Novemba 2017 kabla ya kuwazidi maarifa wageni wao hao 3-0 katika mkondo wa kwanza msimu huu.

Katika mchuano mwingine wa Jumanne katika UEFA, mabingwa watetezi Real Madrid watakuwa wenyeji wa Ajax kutoka Uholanzi uwanjani Santiago Bernabeu.

Real wanaotiwa makali na kocha Santiago Solari watajibwaga ugani wakijivunia ushindi wa 2-1 katika mkondo wa kwanza.

Jumatano itakuwa zamu ya Porto kualika Roma nchini Ureno huku Man-United wakiwaendea miamba wa soka ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), PSG.

You can share this post!

Miradi iliyokwama yageuka silaha dhidi ya Ruto

Jeraha la De Bruyne lamnyima Pep usingizi

adminleo