HabariSiasa

Uhuru hatafaulu kukabili ufisadi – Ripoti

March 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

ZAIDI ya thuluthi mbili ya Wakenya wanaamini kwamba Rais Uhuru Kenyatta hatafaulu kupigana na ufisadi licha ya juhudi zinazoendelea kuukabili, imeonyesha ripoti mpya.

Ripoti hiyo, ambayo ilitolewa na shirika la Twaweza inaonyesha kwamba Wakenya wengi wanaamini kwamba vita hivyo havitafaulu kwani baadhi ya maafisa wakuu wa serikali wamehusishwa na sakata za ufisadi.

Akitoa ripoti hiyo, Mtafiti Mkuu katika shirika hilo Victor Rateng’ alisema kwamba wananchi wengi vilevile wanaamini kwamba kiwango kikubwa cha ufisadi kimetaasisika serikalini, hivyo huenda visifaulu.

“Wengi tuliozungumza nao walieleza tashwishi kuhusu vita hivyo, kwani ni watu wachache waliotajwa kuhusika katika sakata za ufisadi ama kupatikana na hatia waliohukumiwa,” akasema Bw Rateng.

Utafiti huo unajiri wakati viongozi mbalimbali wanaendelea kulaumiana kuhusiana na sakata mpya ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, ambapo inaaminika kwamba huenda serikali imepoteza hadi Sh21 bilioni.

Sakata zingine ambazo zimeikumba serikali ni kupotea kwa Sh1.6 bilioni katika Shirika la Huduma kwa Vijana (NYS), Wizara ya Afya ambapo zaidi ya Sh5 bilioni zinaaminika kufujwa kati ya zingine.

Licha ya hayo, Rais Kenyatta ameapa kukabiliana na zimwi hilo, akiwaagiza Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi (DCI) George Kinoti, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) Twalib Mbarak kuwakabili vikali wale wanaopatikana kuhusika katika sakata hizo.

Thuluthi moja ya Wakenya ilitaja ufisadi kuwa changamoto kuu iliyoiathiri nchi kwa mwaka mmoja uliopita.

Wengi walikubali kuitishwa hongo au kukubali kutoa, ili kupata huduma mbalimbali kutoka asasi za umma.

Utafiti vilevile ulionyesha kwamba thuluthi mbili ya Wakenya wanataja hali ngumu ya maisha kama changamoto kuu zinazowaathiri, kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa kuu za kimsingi kama vyakula.

Hata hivyo, baadhi walieleza kuridhishwa na juhudi za serikali katika sekta za elimu, kuimarisha usalama na usambazaji wa stima.

“Wengi wanasifia juhudi hizo, wakieleza zinachangia sana katika kuimarisha maisha yao kwa kuwawezesha kubuni ajira zaidi,” ikaeleza.

Serikali imekuwa ikiwekeza pakubwa katika sekta ya elimu, baadhi ya malengo makuu yakiwa utekelezaji wa mfumo mpya wa 2-6-6-3. Serikali pia imekuwa ikiweka mikakati ya kulainisha vyuo vikuu na kozi zinazosomesha.

Licha ya changamoto hizo, Wakenya wengi wanamuunga mkono Rais Kenyatta, hasa kutokana na muafaka wake wa kisiasa na Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga.