MAPITIO YA TUNGO: Nargisi Michongomani ni riwaya ya kijazanda inayoanika ukoloni sasa
Mwandishi: Johnson Nzaro
Mchapishaji: One Planet Pulishers
Mhakiki: Wanderi Kamau
Kitabu: Riwaya
Jina la Utungo: Nargisi Michongomani
Kurasa: 235
BAADA ya nchi za Afrika kujipatia uhuru katika miaka ya sitini, mojawapo ya changamoto kuu zilizokabiliana nayo ni uwepo wa viongozi ambao hawakujali maslahi ya raia hata kidogo.
Suala la ugavi wa raslimali asilia kama ardhi lilibaki kuwa fumbo kuu huku viongozi hao wakidhibiti mifumo na taratibu zote zilizotumiwa katika shughuli hizo.
Pengo hilo la kisera ndilo alilolizamia mwandishi Johnson Nzaro kwenye riwaya ‘Nargisi Michongomani’.
Katika riwaya hii yenye usimulizi wa kipekee, mwandishi anaeleza jinsi raia wa nchi ya Zohali walivyojipata watengwa katika nchi yao, chini ya viongozi Weusi, ambao waliwategemea kuwakomboa kutoka kwa manyanyaso ya wakoloni.
Mhusika mkuu, Mvita, anaeleza madhila wanayopitia; kwa mfano kunyang’anywa ardhi yao licha ya kuwa wamiliki halisi.
Sera kandamizi za wakoloni haziwasazi wanawake, kwani nyanyake Mvita alibakwa na kupigwa risasi na askari waliokuwa wakiendeleza dhuluma dhidi ya Waafrika.
Chini ya utawala huo dhalimu, wanaume walikuwa wakilazimishwa kufanya kazi za kijungu jiko katika mashamba ya makaburu wa Kizungu.
Ingawa nchi rejelewa inajipatia uhuru, kungali na matajiri wenye ushawishi ambao wanaendeleza biashara haramu na unyanyanyasaji dhidi wa watu wa tabaka la chini bila kuchukuliwa hatua zozote na serikali iliyopo.
Baadhi yao ni Bwana Swalehe, tajiri wa Kiarabu ambaye anatupa taka ambazo ni sumu kwa viumbe wa majini kama samaki, bila kuadhibiwa na serikali.
Ukatili wake unadhihirika pale anapoagiza kuuawa kwa wafanyakazi wawili (watoto wake Mheshimiwa Mvita, babuye Mvita) wauawe kwa “kukanyaga himaya yake bila ruhusa.”
Wasio na chao wanaumia, hata ikiwa ni werevu. Hii ndiyo hali anayojipata Mvita.
Analazimika kufanya kazi za vibarua kama bawabu, mchungaji, mzegazega, mmachinga kati ya nyingine ili kufanikisha ndoto yake ya kupata elimu.
Hili ni kinyume na watoto kama Lucy (bintiye Swalehe), Nuru (bintiye Askofu Koja) na Smaku ambao wanafanikiwa kupata elimu kwani walitoka katika familia tajiri.
Ni mkasa kwamba nchi nyingi za Kiafrika zina utajiri asilia kama madini na mafuta, ila raia wake wanazidi kuumia, hata kukosa mahitaji ya kimsingi kama elimu.
Watu wenye uwezo (ambao mwandishi anawafananisha na ua la Nargisi) wanazuiliwa na wenye maovu (michongoma) kufikia ndoto zao ili kuwa manufaa kwa jamii zao.
Kama vile ua la nargisi lijizatitivyo kuondoka katika miiba ya michongoma, ndivyo mhusika anavyotia bidii kujikomboa kutoka mazingira yaliyojaa khiana za kila aina.
Kwa ujumla, ni riwaya yenye mafunzo mduara kuhusu masuala muhimu ya uongozi bora, siasa na hata ndoa.
Wasiliana na Mhakiki kupitia baruapepe: [email protected]