• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kiswahili kama lugha ya kufundishia kwa mujibu wa wataalamu

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Kiswahili kama lugha ya kufundishia kwa mujibu wa wataalamu

Na MARY WANGARI

TUNAENDELEA kufafanua mada kuhusu nafasi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia kwa kuangazia wataalamu mbalimbali.

Kulingana na Brock-Utne na wenzake (2005), ni kwamba ujuzi katika lugha ya kufundishia ni jambo muhimu. Hii ni kwa sababu, inawezesha, wanafunzi kuuliza maswali, kujadili na kubainisha mada na wenzao au mwalimu, kufikiri kwa kina namna maarifa mapya yanavyohusiana na yale walio nayo.

Kwa upande mwingine, ukosefu wa umilisi wa lugha ya kufundishia ni kikwazo kikuu kwa wanafunzi kuelewa jinsi ya kuunda maswali, hoja za mijadala na kufikiri kwa kina.

Naye O-Saki (2003), anadai kwamba walimu na wanafunzi wanapofanya kazi katika mazingira ya lugha wasiokuwa na umilisi wake, ni vigumu kuelewana na ni vigumu kwa mwanafunzi kuelewa dhana ya mada iliyofundishwa.

Isitoshe, O-saki anafafanua kwamba, kimsingi umilisi wa lugha ya kufundishia ni njia mojawapo ya kupitishia maarifa ya mfumo wa elimu ya jamii, kanuni za misamiati na utamaduni wa jamii husika.

Rubagumya (2003), anaeleza kuwa walimu wengi wa shule za Sekondari Tanzania hawana uwezo wa kutumia lugha ya Kiingereza kwa ufasaha katika kufundishia; badala yake huchanganya lugha mbili ili waweze kufafanua mada darasani.

Kwa upande wake Rubagumya, anafafanua kwamba wanafunzi wanawaelewa vizuri walimu wao pale ambapo mafunzo hutolewa kwa lugha ya Kiswahili. Aidha, anasema kuwa tatizo huanzia pale wanafunzi wanapoanza elimu ya sekondari bila ya kuwaandaa vya kutosha kukabiliana na matumizi ya lugha ya kigeni.

Kupoteza mwelekeo

Matokeo ya hali hii ni kwamba, wanafunzi wengi huanza kupoteza mwelekeo tangu kidato cha kwanza kwa kutoelewa vizuri masomo kutokana na ushiriki wao mdogo pale wanapofundishwa kwa lugha ya kigeni.

Ni vyema kuelewa kwamba lugha ya Kiswahili imekuwa na ina uwezo mkubwa wa kuweza kupewa dhima ya kufundishia sekondari.

Wasomi tajika Rubanza (1979), Mochiwa (1979), Mekacha (1995) na (1997), wanaonyesha kwamba uelewa wa watoto wengi wa vijijini wanaofahamu Kiswahili kama lugha ya pili umeongezeka. Vilevile, idadi ya watanzania wanaotumia lugha ya Kiswahili kama lugha ya kwanza inaongezeka kwa haraka pia.

 

Baruapepe ya Mwandishi: [email protected]

 

Marejeo

Rugemalira, J. M. (2005). Theoretical and Practical Challenges in a Tanzanian English Medium School. Africa and Asia

Senkoro, F. (2004). The role of language in education and poverty alleviation: Tool for access and empowerment in Justian Galabawa and Anders Narman Education poverty and Inequality (eds.). Dar es Salaam: KAD Associates

Skutnabb-Kangas, T. & McCarty, T. L. (2008). Key concepts in bilingual education: Ideological, historical, epistemological and empirical foundations. In J. Cummins and N. H. Hornberger (Eds.), Encyclopedia of Language and Education, 2nd Edition, Volume 5: Bilingual Education. New York: Springer Science + Business Media LLC.

You can share this post!

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Matumizi ya Kiswahili kama lugha...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya Kiswahili kama lugha...

adminleo