• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
AKILIMALI: Soko la vyakula asili lainua hadhi na thamani ya mihogo

AKILIMALI: Soko la vyakula asili lainua hadhi na thamani ya mihogo

Na GRACE KARANJA

HAPO awali zao la muhogo lilionekana kukuzwa katika familia zilizokumbwa na umaskini lakini katika karne ya leo dhana hiyo imebadilika na kuwa zao la kuliwa na idadi kubwa ya watu ikiwemo walio na mali hivyo kuwa chanzo cha mapato katika jamii.

Muhogo ni mojawapo ya mazao ambayo Wizara ya Kilimo inaendelea kuhamasisha wakulima kutilia maanani hasa katika sehemu ambazo hupokea viwango vya chini vya mvua, wakisema kwamba mmea huu hustahimili ukame.

Gerald Kariuki ni afisa wa kilimo cha mimea kutoka KARLO, katika tawi la Kiambu na Nairobi anasema kuwa mihogo hufanya vizuri sana katika maeneo ya nyanda za chini ambayo hupokea kiwango cha mvua kati ya mm0-mm1, 500 na joto nyuzi 25-30 na sio lazima.

Afisa wa kilimo cha mimea kutoka KARLO tawi la Nairobi akionyesha mimea ya mihogo ambayo bado haijakomaa. Picha/ Grace Karanja

Kulingana naye, muhogo ni mmea wa kipekee na hufanya vizuri sana katika pwani ya Kenya, Magharibi na kati huku baadhi ya wakulima wakiamua kupanda zao hili pamoja na mimea mingine kama kunde na maharagwe.

Hata hivyo, mtaalamu huyu anapinga uzoefu huo na kuwaonya wakulima dhidi ya kuchanganya mimea shambani akisema kufanya hivyo hupunguza mazao.

“Wakulima wawe na uzoefu wa kutenga sehemu za kupanda mimea fulani katika sehemu moja bila ya kuchanganya mimea kwa mingine kwa sababu kufanya hivyo ni kupunguza virutubisho kwenye udongo na kutakuwa na mazao duni, mihogo itakuwa nyembamba. Pia wakati wa kupalilia mimea jirani, huenda mkulima akakata mizizi au hata kukwaruzwa ikizingatiwa kuwa mizizi hii ndio itakuwa mihogo,” anaeleza.

Bw Kariuki anaeleza kuwa, mihogo inahitaji mvua mara mbili pekee ili kuweza kuwa na mizizi imara kisha baadaye kutoa majani na kurefuka hata kama mvua itapungua kwa muda au kukosekana kabisa.

Kuna aina tofauti za mihogo inayokuzwa hapa nchini Kenya kama vile Mucericeri, X-ndogo, KME 1,2,3,4, 61 na EX ndovu ambazo hukua kwenye aina zote za udongo; hasa ule wenye rutuba nyingi, rutuba ya kati na pia ule udongo ambao hauna rutuba.

Kupanda

Muhogo hukatwa vipande vyenye urefu wa kati ya sentimita 15 hadi sentimita 20 na kuwekwa kwenye mtaro wa wastani.

Wakati wa kukata vipande vya mbegu kutoka kwa muhogo wa awali mkulima anashauriwa kuchagua mimea iliyokomaa vizuri, na ambayo haina maambukizi yeyote.

“Kwa kufanya hivyo mkulima atapanda mihogo iliyo na afya ambapo vijisehemu hivyo vinaweza kulazwa ardhini, kusimamishwa wima au kuinamishwa na kisha kufunikwa kwa mchanga mwepesi ili kuchipuka haraka,” anaeleza Bw Kariuki.

Kijiti kimoja hupandwa na kuwachwa nafasi ya mita moja kwa moja kutoka mmea mmoja hadi mwingine na vipimo vivyo hivyo kutoka mstari mmoja hadi mwingine.

Kulingana na mtaalamu huyu, muhogo huhitaji mchanga mwepesi.

Kumbuka kwamba baada ya kupanda na mmea kuanza kuonyesha dalili ya kuota, sambaza mbolea ya samadi kando ya mmea wa muhogo ili kuifanya mizizi kupata rutuba ya kutosha.

Hata hivyo Bw Kariuki anaongeza kuwa kupalilia mimea ni muhimu zaidi kwa kuwa mkulima atapunguza uwezakano wa mimea kushambuliwa na wadudu waharibifu.

Muhogo huchukua muda wa miezi 9 hadi 16 ili kuwa tayari na kuvunwa. Uvunaji mapema wa mihogo unaweza kuwa na faida hasa wakati wa jua hivyo kuepuka hasara itokanayo na magonjwa.

You can share this post!

AKILIMALI: Kunasa na kuandaa kumbikumbi humpa kipato

AKILIMALI: Mradi wa biogesi wapunguza gharama ya kuni shule...

adminleo