UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Vikwazo vinavyokabili Kiswahili kama lugha ya kufundishia
Na MARY WANGARI
JINSI tulivyogundua, lugha ya Kiswahili ina nguvu ya kuwapa watumiaji wake uwezo wa kutumia teknolojia kufanyia mambo yao na wala si yale yenye asili ya kigeni tu.
Msanjila na wenzie (2009) wanahitimisha kwa kusema kwamba, mafanikio haya kwa jamii yanakiweka Kiswahili katika nafasi nzuri ya kupewa nafasi ya kutumika katika elimu ya sekondari kama zilivyopewa hizo lugha sita kubwa zilizopiga hatua kisayansi na kiteknolojia.
Nafasi kama hiyo itaipa lugha hii fursa mpya ya kuweza kutumiwa pia kujenga maendeleo ya jamii kwenye misingi ya kiutamaduni ya jamii ya nchi ya Tanzania.
Senkoro (2004), anatoa hoja kwamba, pamoja na serikali kuchochea kwake kuanzishwa kwa vyombo rasmi vya kuendeleza lugha ya Kiswahili, haikuandamana na sheria ya kutilia mkazo utekelezaji wa matakwa na mahitaji ya lugha ya hadhi hiyo, ambayo ni pamoja na kufundishia elimu za viwango vyote.
Kikwazo kingine ni kuchelewa kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia elimu ya sekondari.
Ripoti ya Tume ya Makweta ya 1982, ilipendekeza kwamba Kiswahili kianze kutumika kama lugha ya kufundishia elimu ya sekondari kuanzia mwaka 1985.
Kabla ya mpango huo kutekelezwa serikali ilitoa mwongozo kwamba Kiingereza kiendelee kutumika katika sekondari na vyuo. Tamko hilo limezua mjadala ambao unaendelea hadi leo nchini Tanzania.
Ni bayana kwamba tangu iliyokuwa Tanganyika ipate Uhuru, jitihada nyingi zimeshafanyika za kukifanya Kiswahili kiwe lugha ya kufundishia elimu ya sekondari lakini bado hakujawa na mafanikio ya kiutekelezaji mpaka sasa.
Naye Qorro (2003) anaeleza kwamba lugha ya kwanza huwa ni chombo cha kumwezesha mtumiaji kung’amua na kueleza mtazamo na hisia zake za ndani kwa kila kinachomfikia au kinachotolewa kwake.
Uwezo huu wa kung’amua na kueleza mtazamo na hisia za ndani kuhusu maarifa, ndiyo msingi wa ubunifu na ugunduzi.
Nchini Tanzania, lugha ya Kiswahili ni ya kwanza kwa baadhi na ni ya pili kwa baadhi ya wananchi.
Hata hivyo, lugha inayotumika kufundishia elimu ya sekondari ni ya tatu kwa wananchi walio wengi. Hali hiyo husababisha walimu kukosa uwezo unaostahili wa kufundisha masomo ya sekondari.
Baruapepe ya mwandishi: [email protected]
Marejeo
Kothari, C. R. (2004). Research methodology Methods and Techniques (2nd ed.). New Delhi: New Age International Publishers.
Koul L. (2009). Methodology of Educational Research ( 4th ed.). New Delhi: Inda Vikas Publishing House PVT Ltd.
Lambert, W. E. na wenzie (1960). “Evaluational Reactions to Spoken Languages”. Journal of Abnormal and Social Psychology. 20.1