• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Kabati Youth FC yaongoza Aberdare Regional League Kundi A

Kabati Youth FC yaongoza Aberdare Regional League Kundi A

Na LAWRENCE ONGARO

KIKOSI cha Kabati Youth FC kinaendelea kuongoza Ligi ya Aberdare Regional League Kundi A, kikiwa na alama 13 baada ya kucheza mechi tano tangu mechi hizo zing’oe nanga kipindi cha miezi miwili iliyopita.

Timu hiyo imeshinda mechi nne na kutoka sare mechi moja, bila kupoteza mechi yoyote.

Vijana hao wanatoka eneo la Kabati, Kaunti ya Murang’a.

Kocha Stephen Odhiambo anasema ya kwamba vijana wake wamekuwa na ushirikiano mzuri naye na ndiyo maana wanaendelea kuwatesa wapinzani wake.

“Mazoezi yetu hufanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Mukerenju, Murang’a na kila mchezaji hujituma kufika mazoezini bila kushurutishwa. Hii ni njia moja ya kuweka timu kuwa imara kabisa,” amesema Odhiambo.

Katika mechi ya juzi, vijana wa Kabati Youth waliirarua Jungle Nuts FC kwa mabao 2-1.

Mkufunzi alisema kikosi chake kipo imara lakini anapanga kufanya marekebisho machache katika kiungo cha kati ambacho anasema kina ulegevu kidogo.

“Ninaelewa vyema kuwa nina ushindani mkali kutoka timu kadha tunazoshindana nazo, lakini lengo langu kuu ni kuona ya kwamba ninatafuta mbinu ya kukabiliana nao ili niendelee kubaki kileleni,” alisema Odhiambo.

Klabu ya Muchatha inafuata katika nafasi ya pili ikiwa na alama 12. Timu hiyo imeweza kujitupa dimbani kwa mechi nne. Katika hali hiyo, imeshinda mechi nne lakini hawajatoka sare mechi yoyote wala kushindwa.

Katika mechi iliyochezwa juzi, timu hiyo iliibana Ngecha FC ya Limuru kwa bao 1-0.

Wanasoka wa Destiny wanajivunia kuwa kwenye nafasi ya tatu wakiwa na pointi tisa. Timu hiyo imecheza mechi nne na kushinda tatu. Vijana hao hawajatoka sare yoyote, lakini wamepoteza mechi moja pekee.

Timu ya Angaza ya kocha Victor Kabanji inakamata nafasi ya nne ikiwa na alama saba.

Vijana hao wamecheza mechi nne na kushinda mbili. Katika patashika hiyo, wametoka sare mechi moja na kushindwa moja.

Timu ya Thika Cloth Mills (TCM), inafunga jedwali la tano bora na alama saba baada ya kucheza mechi tano na kushinda mbili.

Katika hali hiyo, wametoka sare moja na kupoteza mbili.

Kocha wake Robert Wafula anasema atalazimika kutumia mbinu geni ili kukabiliana na wapinzani wake huku lengo lake likiwa kukamilisha mzunguko wa ligi katika tatu bora.

You can share this post!

Timu ya voliboli ya KCB yaenda Misri kupigania ubingwa wa...

‘Githeri Man’ hufuga kuku wa kienyeji, japo si...

adminleo