Duru mpya ya Kakamega Sevens yaongezwa katika raga za kitaifa
Na GEOFFREY ANENE
DURU mpya ya Kakamega Sevens imejumuishwa kwenye Raga za Kitaifa za wachezaji saba kila upande, ambazo ratiba yake ya mwaka 2019 imetangazwa Ijumaa.
Kakamega Sevens, ambayo inaingia katika mashindano haya yanayofanyika kila mwaka tangu mwaka 1999, imejaza nafasi ya duru ya Sepetuka Sevens, ambayo imeondolewa.
Duru ya Kakamega itakuwa ya kwanza kuandalia. Timu zitashindania taji mnamo Julai 20-21, wenyeji wakiwa timu ya Western Bulls, ambayo ilitemwa kutoka Ligi Kuu misimu miwili iliyopita, na mabingwa wa Kenya mwaka 2016 Kabras Sugar. Bulls na Kabras zinatoka katika kaunti ya Kakamega.
Mwaka 2017, klabu ya Homeboyz iliomba kuandaa duru moja kwa kipindi cha miaka miaka. Homeboyz ndio ilikuwa mwenyeji wa Sepetuka Sevens mwaka 2017 na 2018 mjini Eldoret. Ombi la pamoja kutoka kwa Kabras na Bulls litashuhudia Kakamega ikiwa mwenyeji wa Kakamega Sevens mwaka 2019 na 2020.
Baada ya kuzuru Kakamega, timu zitaelekea jijini Nairobi kwa duru ya pili ya George Mwangi Kabeberi Sevens uwanjani RFUEA Grounds. Duru hii ambayo mwenyeji wake ni klabu ya Mwamba, inarejea jijini baada ya kuandaliwa mjini Machakos mwaka 2018. Mwaka huu itafanyika Julai 27-29. Raga hii kisha itachukua likizo Agosti 3-4 kabla ya kuendelea Agosti 10-11 ambapo mji wa Kisumu utaandaa Dala Sevens uwanjani Mamboleo Showground ASK.
Duru ya Prinsloo itafuatia mnamo Agosti 17-18 mjini Nakuru kabla ya Kenya Harlequins kuandaa Christie Sevens uwanjani RFUEA Grounds na kisha duru ya Driftwood Sevens kufunga mwaka mnamo Septemba 7-8 mjini Mombasa.
Homeboyz ndio mabingwa watetezi. ‘Madeejay’ hawa walishinda Prinsloo, Kabeberi, Sepetuka na Christie. Mwamba ilimaliza katika nafasi ya pili baada ya kufika fainali tatu na kutwaa taji la Dala Sevens.
Ratiba ya mwaka 2019
Julai 20-21: Kakamega Sevens, Bull Ring Kakamega
Julai 27-28: Kabeberi Sevens, RFUEA Grounds
Agosti 3-4: Mapumziko
Agosti 10-11: Dala Sevens, Mamboleo Showground ASK
Agosti 17-18: Prinsloo Sevens, Nakuru Athletics Club
Agosti 24-25: Mapumziko
Agosti 31 na Septemba 1: Christie Sevens, RFUEA Grounds
Septemba 7-8: Driftwood Sevens, Mombasa Sports Club
Washindi wa raga za kitaifa
1999 Impala Saracens
2000 Impala Saracens
2001 Impala Saracens
2002 Ulinzi
2003 Ulinzi
2004 Impala Saracens
2005 Kenya Harlequin
2006 Kenya Harlequin
2007 Mwamba
2008 Mwamba
2009 Strathmore Leos
2010 Mwamba
2011 Mwamba
2012 Kenya Harlequin
2013 KCB
2014 KCB
2015 Nakuru
2016 Homeboyz
2017 Kabras Sugar
2019 ?