Kadhia ya moto mitaa ya mabanda Nairobi
Na SAMMY KIMATU
WATU zaidi ya 3,000 walilazimika kukesha nje penye baridi baada ya nyumba 1,000 kuteketea Ijumaa usiku katika mitaa miwili ya mabanda ya Mukuru ilioko South B, Kaunti ya Nairobi.
Katika kisa cha kwanza mtaani Mukuru-Maasai katika lokesheni ya Mukuru-Nyayo, nyumba 400 houses ziliteketea baada ya moto kuanza mwendo saa saba unusu.
Bw Joshua Mue, 32, mfanyakazi katika Kaunti ya Nairobi alisema moto ulianza katika nyumba moja mwanamke alipoacha kifaa cha stima cha kuchemshia maji pekee bila mtu ndani ya nyumba.
Moto uliongezwa na upepo mkali na pia milipuko ya mitungi ya gesi baada ya kusambaa hadi nyumba zingine.
Biashara zikiwemo bucha, saluni na vibanda vya mboga viliungua katika mkasa huo.
Mwathiriwa mwingine, Veronicah Mangu, 26, alisema mwanawe John Wendo,1, alichomeka kichwani, mguuni na mkononi wakati wa kuokoa mali.
Mumewe, Nicodemus Mutisya, 33, anayefanya na kampuni ya Standard Gauge Railway (SGR) aliarifiwa kuhusu moto kwa kupigiwa simu.
Magari matatu ya kuzima moto yalishindwa kuingia katika eneo la mkasa baada ya kukosa njia na kulazimika kuingia ndani ya mtaa wa Hazina.
Mwathiriwa mwingine, Agnes Wanjala, 42, mama wa watoto sita alisema nguo zote aina ya vitenge ziliteketea kabisa zikiwa ndani ya nyumba. pamja na nguo na vitabu vya wanawe
Mwenyekiti wa mtaa huo, Bw Charles Nyamwega, 67,anaomba wasamaria wema kusaidia wakazi walioathirika.
Katika kisa cha pili, nyumba 600 ziliteketea kuanzi mwendo wa saa mbili unusu katika mtaa wa Mukuru-Commercial ulioko katika tarafa ya Land Mawe.
Inadaiwa mwanamume alikuwa akiunganisha nyaya za stima kinyume cha sheria.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Bw Onesmus Muteti Kisengese alisema polisi wanamtafuta kwa udi na uvumba mshukiwa kwa jina “Kanjero” aliyetoroka baada moto kuwaka.
Viongozi
Mwakilishi wa wadi wa eneo hilo, Bw Herman Azangu, pamoja na wasimamizi kadhaa wa mitaa ya mabanda ya Land Mawe walifika katika eneo la mkasa usiku huo.
Mbunge wa Starehe Bw Charles Njagua Kanyi alihahidi msaada wa chakula na vingine vitakavyopatikana ndiposa waathiriwa wasaidiwe.
Wiki jana, watu watatu walifariki huku nyumba 600 zikiteketea katika mtaa huo wa Mukuru-Commercial.
Katika tukio la jana, moto ulimalizia kabisa nyumba zilizobakia katika moto wa wiki jana na kuwaachwa wakazi wakishangaa.