Super Solico na St Marys Ndovea mabingwa wa Chapa Dimba Mashariki
Na JOHN KIMWERE
SUPER Solico FC na St Marys Ndovea zimeibuka wafalme na malkia wa Chapa Dimba na Safaricom Season Two, Mkoani Mashariki mtawalia baada ya kutesa wapinzani wao kwenye fainali zilizochezewa uwanjani Kitui Show Ground.
Super solico FC iljipatia ushindi huo ilipotandika wenzao wa Isiolo Young Stars mabao 4-3 kupitia mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida.
Nao wasichana wa St Marys Ndovea walibeba umalkia huo walipoandikisha ufanisi wa mabao 2-1 mbele ya Chuka Starlets. Clare Chemutai alitangulia kufungia Chuka Starlets dakika ya pili kabla ya St Marys Ndovea kusawazisha kupitia Margaret Mutua dakika 33 baadaye. Hata hivyo kunako dakika ya 57 Cecilia Mutungu aliachia kombora zito kimiani lililosaidia St Marys ndovea kuzoa tiketi ya fainali.
”Tunashukuru Mungu maana tumetimiza ndoto yetu kufuzu kwa fainali za kitaifa,” nahodha wa St Marys Ndovea Margaret Mutua alisema. Kitengo cha wavulana Supersolico ilitangulia kufunga kupitia James Mutua kabla ya Ibrahim Abdisalan kusawazishia Isiolo Young Stars.
”Tuna furaha tele kunasa tiketi ya kuwakilisha mkoa huu katika fainali za kitaifa,” kocha wa Super solico Mudachi Bernard alisema. Kando na tiketi ya fainali washindi hao kila mmoja alituzwa Sh200,000. Mabingwa hao wamejiunga na wenzao Lungari Blue Saints (wavulana) na Bishop Njenga (wasichana) kutoka Mkoa wa Magharibi, Manyatta Boys na Ndhiwa Queens, wavulana na wasichana mtawalia kutoka Mkoa wa Nyanza.