• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 11:34 AM
Miguna Miguna: Raila ndiye aliniambia Jubilee ilimpa Magaya Sh30 milioni

Miguna Miguna: Raila ndiye aliniambia Jubilee ilimpa Magaya Sh30 milioni

Na BENSON MATHEKA

WAKILI mbishi Miguna Miguna sasa amedai kwamba kinara wa NASA, Raila Odinga, alimweleza binafsi kwamba Afisa Mkuu wa muungano huo Norman Magaya, alipokea Sh30 milioni kutoka kwa chama cha Jubilee. 

Akihojiwa na kituo cha runinga cha TRT World jijini Toronto, Canada mnamo Jumanne usiku, Bw Miguna alikanusha madai kwamba anampiga vita Bw Odinga na viongozi wengine wa NASA.

“Ni kweli Bw Magaya alipokea Sh30 milioni kutoka kwa Jubilee ndipo aondoe kesi ya kupinga ushindi wa gavana wa Nairobi. Raila Odinga mwenyewe alinifahamisha hayo,” alidai Bw Miguna.

Wiki iliyopita, Bw Miguna alimlaumu Bw Magaya na mwanamikakati wa NASA, David Ndii, akisema wanatumiwa na Jubilee kuvuruga NASA. Alidai kwamba Bw Ndii alipinga kuapishwa kwa Bw Odinga kuwa “rais wa wananchi”.

Siku iliyofuata Bw Odinga aliwatetea maafisa hao akisema wanatekeleza wajibu muhimu katika NASA na kuwataka wafuasi wa muungano huo kumpuuza Bw Miguna.

Lakini wakili huyo aliambia kipindi cha Newsmakers cha runinga ya TRT World kwamba kwa kumpuuza, Raila anahatarisha hatima yake ya kisiasa.

 

‘Huwezi kunipuuza’

“Huwezi ukampuuza Bw Miguna. Hata Raila Odinga hawezi. Vijana walio Nairobi hawatakusikiliza, vijana wa Kenya hawatakusikiliza, kwa sasa wanamwamini sana Miguna Miguna,” alisema.

Alisema serikali ya Jubilee ilimfukuza nchini kwa sababu inafahamu ushawishi wake wa kuongoza raia kudai haki.

“Jubilee wanajua kwamba sisemi jambo nisiloweza kutimiza. Nilisema nitamuapisha Bw Odinga na nikafanya hivyo mbele ya mamilioni ya watu.

Nilipowataka Wakenya kuchoma picha za Rais Kenyatta, nilikamatwa na kuzuiliwa kwa wiki moja kinyume cha sheria kabla ya kutimuliwa pia kinyume cha sheria,” alisema.

Alisisitiza kuwa atarejea Kenya mwezi ujao kuendeleza kampeni ya vuguvugu lililoharamishwa la NRM.

“Ninatarajia kurudi Kenya mwezi ujao baada ya kuzuru miji ya hapa Canada, Amerika, Uropa, Uarabuni na Afrika,” alisema Bw Miguna.

 

 

You can share this post!

Afikishwa kortini bila viatu kwa kuiba mtoto

Kijana aliyetoroka Al Shabaab asimulia maisha yalivyokuwa...

adminleo