• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 3:03 PM
K’Ogalo yasukumwa hadi mkiani Zamalek ikipepea

K’Ogalo yasukumwa hadi mkiani Zamalek ikipepea

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Kenya Gor Mahia, wanakabiliwa na hatari ya kuaga Kombe la Mashirikisho la Afrika baada ya kutamatisha ziara yao ya kaskazini mwa Afrika kwa kukaangwa 4-0 na Zamalek mjini Alexandria, Jumapili.

Vijana wa Hassan Oktay, ambao waliongoza Kundi D kabla ya ziara hiyo iliyoanza na kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Hussein Dey nchini Algeria mnamo Machi 3, sasa wako mkiani kwa alama sita.

Gor, ambao mara ya mwisho walialikwa na Zamalek walipepetwa 4-0 Aprili 5, 1998, katika raundi ya kwanza ya kipute hiki, wako katika ulazima wa kuchapa nambari mbili Petro de Luanda kutoka Angola mnamo Machi 17 jijini Nairobi ndiposa wasalie mashindanoni.

Matokeo mengine yasiyo ushindi yatashuhudia Gor ikibanduliwa nje.

Zamalek, ambayo ilianza kampeni yake kwa kucharazwa 4-2 na Gor jijini Nairobi mnamo Februari 3 na kumaliza mechi tatu za kwanza bila ushindi, imechukua usukani kwa alama nane baada ya waliokuwa viongozi Hussein Dey pia kupoteza 2-0 dhidi ya Petro jijini Luanda.

Miamba hawa wa Misri walizamisha chombo cha Gor mnamo Jumapili usiku kupitia mabao ya Mahmoud Alaa, Youssef Obama, Ferjani Sassi na Omar El Said.

Alama moja

Zamalek wako alama moja mbele ya Petro na Hussein Dey.

Baada ya kulemewa na Zamalek, mashabiki wengi wa Gor walikubali timu yao ilikimbiza vivuli tu uwanjani.

Pia, walilaumu viongozi wa klabu kuuza mshambuliaji matata kutoka Rwanda Meddie Kagere na beki Mganda Godfrey Walusimbi “wakijua Gor itashiriki mashindano ya Bara Afrika.”

Vilevile, walikiri kwamba kukosekana kwa kiungo Mganda Shafik Batambuze na kutotumiwa kwa mshambuliaji Nicholas Kipkirui kulichangia pakubwa katika ziara mbovu ya Gor nchini Algeria na Misri.

Batambuze alikuwa nje akitumikia marufuku ya mechi moja kwa kuonyeshwa kadi mbili za njano.

Nayo Nkana, ambayo imeajiri Wakenya Musa Mohamed na Duncan Otieno, ilijiweka pazuri kuingia robo-fainali baada ya kulemea Zesco United ambayo imeajiri Wakenya Jesse Were, Anthony Akumu na David Owino, 3-0.

Zesco iko mkiani. Imeaga mashindano.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Wangu wa kwanza ameniharibia sifa kwa...

NI KISASI: Atletico kwenye mizani ya Juventus huku City...

adminleo