• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Yakujuzu kufahamu haya kuhusu kilimo cha tufaa

Yakujuzu kufahamu haya kuhusu kilimo cha tufaa

Na SAMMY WAWERU

KENYA ina upungufu wa matufaha kwani kwa mwaka hununua zaidi ya tani 10,000 za matunda haya kutoka nje ya nchi.

Mataifa yanayoyapanda kwa wingi ni kama vile; China ambayo inaongoza kwa karibu tani milioni 37.

Inafuatwa na Marekani inayozalisha tani milioni 4.11 na Uturuki tani milioni 2.88.

Nchi zingine katika orodha hii ni; Poland tani milioni 2.87, India (2.20), Italia (1.99) na Brazil (1.81).

Barani Afrika mataifa yanayokuza matunda haya kwa wingi ni; Misri, Morocco, Afrika Kusini, Tunisia na Nigeria.

Bw Peter Wambugu, ambaye ni mkulima tajika wa matufaha nchini anasema matunda haya ni miongoni mwa yale rahisi mno kupanda na kutunza.

Mkulima huyu ndiye mwasisi wa Wambugu Apples, matufaha yanayoanza kuvunwa miezi tisa baada ya upanzi.

Matufaha mengine huanza kuvunwa baada ya miaka miwili.

Raslimali

Bw Wambugu aliyavumbua mwaka 2014, kupitia utafiti wa aina yake.

Aidha anasema yanahitaji mbolea na maji pekee kuyakuza.

“Kenya ni taifa lililojaaliwa kwa raslimali nyingi, kuanzia mchanga wenye rutuba hadi maji hivyo basi sekta ya kilimo ni rahisi kufanikisha. Upungufu wa matunda haya unaoshuhudiwa unaweza ukawa historia endapo wakulima watakumbatia matufaha kwa kuwa hayana kazi kuyapanda na kutunza,” anaeleza Bw Wambugu. Anaongeza, “Ukiyalisha kwa mbolea na maji, kilimo cha matufaha ni dhahabu.”

Wazalishaji wa matunda haya nchini ni wachache mno na kwa mujibu wa maelezo ya Mzee Wambugu, Wambugu Apples yanastawi katika maeneo yenye joto.

Aidha, matufaha yanaaminika kukua vyema maeneo ya baridi.

Kulingana na James Macharia, mtaalamu wa masuala ya kilimo mazingira ya baridi husaidia mitofaha kupukutua majani, ili ianze kuchana maua. “Maua yachanapo huzalisha matunda,” anasema Bw Macharia.

Matufaha ya Wambugu hustawi maeneo ya joto na baridi.

Laikipia hupokea kiwango cha juu cha joto, ikizingatiwa kuwa ni eneo linaloshuhudia kiangazi na ndiko mkulima huyu anayakuza.

Namna ya kuyapanda

Wambugu Apples ni ya kupandikiza, shughuli ambayo huchukua muda wa miezi miwili kitaluni.

Catherine Nyokabi Wambugu, meneja wa mauzo na matangazo na ambaye pia ni binti ya Bw Wambugu anasema mashimo ndiyo hutumika kuyapanda.

Catherine Nyokabi Wambugu, meneja wa mauzo na matangazo Wambugu Apples, akionyesha miche ya matufaha iliyopandikizwa shambani. Picha/ Sammy Waweru

“Shimo liwe na upana wa futi 2, na urefu wa kipimo sawa na hicho kuenda chini,” aeleza Bi Nyokabi.

Mzee Wambugu anasema kipimo cha shimo hadi lingine kiwe futi 8 au mita 3, mraba.

Anaendelea kueleza kwamba mbolea huchanganywa na mchanga uliochimbwa wa sehemu ya juu, mchanganyiko huo unarejeshwa shimoni kimo cha futi moja.

Mkulima anahimizwa kuweka maji kabla ya kupanda mche.

“Futi moja iliyosalia ni ya kutunza mtofaha kwa mbolea na maji,” asema Wambugu.

Matunzo

Kupalilia kuondoa makwekwe ni shughuli muhimu katika kilimo.

Wambugu anasisitiza kuitilia maanani kwani makwekwe hula chakula cha mimea, ambayo ni; pembejeo na maji. Wakati wa mahojiano alisema matunda ya Wambugu Apples ni nadra kuathiriwa na wadudu na magonjwa.

Miezi tisa baadaye, matufaha haya huwa tayari kuvunwa.

Wambugu Apples imeidhinishwa na taasisi ya kitaifa ya utafiti wa kilimo na ufugaji nchini (Karlo) na ya ubora wa mimea (Kephis).

Kulingana na Bw Daniel Mwenda, mtaalamu wa kilimo haswa matunda utafiti wa mimea huchukua karibu miaka miwili.

You can share this post!

“Nilikasirika sana nilipofungiwa nje ya ndege ya mauti...

VIDUBWASHA: Kitakufaa msimu wa baridi (Nicelucky Coffee Mug...

adminleo