Habari

Kadinali aliyedhulumu watoto wavulana atupwa jela miaka sita

March 13th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA  

MHUBIRI wa kikatoliki na mwandani wa kiongozi wa kanisa hilo Papa Francis kutoka Australia ambaye majuzi alipatikana na hatia ya kuwadhulumu wavulana wawili kingono zaidi ya miaka 20 iliyopita ametupwa jela miaka sita.

Kadinali George Pell, 77, alipatikana na makosa ya kuwadhulumu watoto hao kingono, kwa kuwafanyia ‘ngono ya mdomo’ katika kanisa la St Patricks Cathedral, Jijini Melbourne baada ya misa ya kanisa.

Wavulana hao walikuwa waimbaji wa kwaya.

Huyo sasa anakuwa afisa wa kwanza wa ngazi ya juu zaidi katika kanisa hilo kuhukumiwa kwa makosa ya kudhulumu watoto kingono katika kanisa hilo, kwani alikuwa mshauri wa papa.

Jaji Kidd Jumatano alimhukumu kadinali huyo, akisema anaweza kukufia jela.

Jaji huyo alitaja makosa ya Pell kuwa mabaya sana, akisema dhuluma zake ziliwaathiri watoto hao hadi katika ukubwa wao. Hata hivyo, alisema kulingana na umri wake sasa na hali kuwa hajafanya makosa ya aina hiyo tena kwa miaka 22 iliyopita, hakuna uwezekano mkubwa kuwa atarudia tena.

Aidha, jaji huyo alizingatia hali mbaya ya kiafya ya mhubiri huyo kwani ana ugonjwa wa moyo na kupanda presha ya damu, ndipo akasema kuna uwezekano akafariki jela.

Lakini kwa kuwa kadinali huyo bado anapinga kufanya makosa hayo na anapanga kukata rufaa, jaji alisema kuwa hakuonyesha kujutia matendo yake, kwani hilo lingemsaidia kupunguza kifungo.

Mwekahazina

Hadi Februari, Pell alikuwa mwekahazina katika makao makuu ya katoliki Vatican na alikuwa akitarajiwa kuwa papa atakayefuata.

Baada ya kusomewa hukumu, Pope aliondolewa mahakamani na maafisa watano wa jela.

Wadhulumiwa wa makosa ya kingono waliokuwa nje ya mahakama hiyo walishangilia baada ya hukumu hiyo dhidi ya kadinali Pell.

Hata hivyo, wanaharakati walitaja kifungo hicho kuwa cha huruma.

“Hakitoi onyho lolote kwa watu wanaodhulumu wengine kingono, hakitoi ishara ya haki kwa wadhulumiwa,” akasema wakili wa mdhulumiwa Michael Advocate.

Visa hivyo dhidi ya wavulana wawili vilifanyika 1996 na 1997.

 

Imetayarishwa na PETER MBURU