Michezo

Waliodanganya umri katika mchujo sasa watemwa nje

March 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA WAANDISHI WETU

CHAMA cha Riadha cha Kenya (AK) kimewafurusha kikosini watimkaji wawili chipukizi waliokuwa wakijiandaa kwa mbio za Dunia za Nyika zitakazofanyika jijini Aarhus, Denmark mnamo Machi 30.

Makamu Rais wa AK, Paul Mutwii ambaye anasimamia kivumbi hicho, amesema kwamba wawili hao ni Kibet Kandie na Agnes Mwikali waliokuwa katika vikosi vya wavulana na wasichana mtawalia.

Kulingana na Mutwii, kufurushwa kwa wawili hao kulichangiwa na udanganyifu wa umri wakati wa mchujo wa kitaifa ulioandaliwa mjini Eldoret mwishoni mwa Februari.

Nafasi zao kwa sasa zimetwaliwa na Cleophas Kandie na Mercy Cherop mtawalia.

Cleophas aliibuka mshindi wa nishani ya fedha katika mbio za mita 2,000 kuruka maji na viunzi kwenye Riadha za Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 mnamo 2017.

“Kibet alikuja kushiriki mchujo akiwa na cheti cha kuzaliwa kilichoashiria kwamba alikuwa na umri wa miaka 18. Hata hivyo, hakuwa na kitambulisho cha kitaifa,” akatanguliza Mutwii.

“Stakabadhi za Mwikali hazikuwa na uwezo wa kubainisha umri wake kamili. Hivyo, AK ilifikia maamuzi ya kuijaza nafasi yake wakati ikiendelea na uchunguzi zaidi,” akasema kinara huyo.

Mwikali aliambulia nafasi ya nne kwenye mchujo wa kitaifa uliomshuhudia Kibet akifunga orodha ya sita-bora katika kitengo chake na hivyo kujikatia tiketi za kuwakilisha Kenya jijini Aarhus mwishoni mwa Machi 2019.

Cleophas aliteguka na kuanguka katika mzunguko wa mwisho wakati wa mchujo wa kitaifa ulioandaliwa katika uwanja wa Eldoret Sports Club mnamo Februari 23. Cherop kwa upande wake, aliambulia nafasi ya nane.

“Cleophas alikuwa katika nafasi ya tatu wakati alipoteguka na kujiondoa mbioni. Hii ndiyo sababu ya AK kumpa nafasi,” akasema.

Mutwii kwa kusisitiza kwamba walifikia maamuzi ya kumteua Cherop kwa kuwa Roselida Jepketer aliyeambulia nafasi ya saba ana jeraha.

Vyeti ghushi

Mwishoni mwa mchujo, kuliibuka tetesi kwamba baadhi ya wanariadha waliowahi kuwakilisha taifa katika mashindano ya awali katika vitengo vya chipukizi walijitokeza kwa mara nyingine na vyeti ghushi vya kuzaliwa.

Kulingana na Mutwii, mwanariadha wa pekee ambaye hajafika kambini kufikia sasa ni bingwa wa dunia na Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 5,000, Hellen Obiri ambaye atawakilisha Kenya katika mbio za kilomita 10 nchini Denmark.

Obiri hata hivyo alipata idhini ya kuchelewa kuripoti kambini kwa kuwa ana majukumu mengine katika Kamati ya Kitaifa ya Olimpiki (NOC-K).

Obiri ndiye nahodha wa Team Kenya itakayoshiriki makala ya kwanza ya michezo ya ANOCA Zone V Genocide Memorial jijini Kigali, Rwanda mnamo Aprili 2-6, 2019.

Kikosi cha wanariadha wengine 29 walioteuliwa na AK wamekuwa wakijinoa katika Chuo cha Walimu cha Kigari, Embu kuanzia Machi 1.

Bingwa wa Dunia kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 katika mbio za mita 5,000 Beatrice Chebet na Samuel Chebole waliibuka washindi wa vitengo vyao wakati wa mchujo. Wanatarajiwa kutia fora zaidi nchini Denmark.