Makala

AKILIMALI: Mashine ya kisasa inayokata nyasi kwa kasi

March 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MAOSI

Kulingana na utafiti,  nyasi huzoea kumea  mazingira mbalimbali kulingana na ekolojia na tabianchi.

Inasemekana nyasi ndio idadi kubwa ya mimea inayopatikana ulimwenguni, kwa sababu ndio mmea unaoweza kustawi sehemu nyingi duniani.

Malisho mabichi mathalan Napier grass na matawi ya viazi vitamu huwa na maji mengi,pamoja na virutubisho vya kutosha.

Nyasi zinapotumika kwa manufaa ya mkulima, zinafaa kutunzwa vizuri ili kuzihakikishia ubora.

Aidha kuna njia mbalimbali za kuimarisha nyasi, kwa mfano mkulima anaweza kuzikata ili kupatia nafasi zingine kuchipuka.

Kwa upande mmoja nyasi huwa na mizizi mirefu, inayopenyeza baina ya udongo na kushikilia ardhi vyema ili kupunguza uwezekano wa mmomonyoko wa udongo.

Wakulima wadogo wamekuwa wakitumia nyasi kutekeleza shughuli mbalimbali,kama vile lishe kwa mifugo wao yaani kondoo, mbuzi na ng’ombe.

Makasi imekuwa ikitumika kukata majani au nyasi, lakini uvumbuzi wa teknolojia umeibua mtambo mpya wa kukata nyasi.

Sio wakulima wengi wana ujuzi wa kutumia mashine hii, kukata nyasi au majani kwa ajili ya mifugo wao wa nyumbani.

Ni mtambo unaoweza kupunguza idadi ya majani kwenye mashina ya miti au mimea midogo yenye manufaa inayokua katika bustani.

Mtaalam Nicholas Sinda kutoka taasisi ya kutadhmini ubora wa mimea, Kenya Agricultural Research Organisation,anawahimiza wakulima kukumbatia teknolojia ya kilimo.

Akiwa mjuzi wa mimea sampuli ya nyasi, anaelezea haja kubwa ya kutunza raslimali hii ambayo imekuwa ikipuuzwa kwa muda.

Anahimiza kuwa wakulima watapata faraja tele endapo watajifundisha, kunadhifisha nyasi.

Akionesha matumizi ya mashine hii, alisema ni kifaa chenye ncha kali kinachoweza kuvutwa kwa trekta kutekeleza kazi ya kulainisha shamba la nyasi.

Mtambo wenyewe umekazwa na unaweza kufanya kazi mbili kwa wakati mmoja,yaani kukata na kulainisha nyasi.

Anasema ‘cutter’ inaweza kupunguza idadi kubwa ya nyasi,z ilizorundikana shambani kwa muda maalum na kupunguza mzigo wa kasi ya mikono.

“Mashine hii huweza kupunguza majani makavu katika shina ,kwa kuzingatia utaratibu wake ambapo mwekezaji hahitajiki kutegemea vibarua,”alisema.

Sio tu kuokoa muda, bali matokeo yake ni ya kuridhisha ikizingatiwa cutter hulainisha nyasi za mkulima baada ya kuzikata.

Masine hii huunganishwa kwa trekta inayozungusha visu vyenye umbo la duara,na kupunguza urefu wa nyasi.

Nyasi za napier hukua kwa kasi pindi tu baada ya kupogolewa kwani hupata fursa ya kukua upya na kupatia mikunde fursa ya kuchipuka.

Nicholas anasema kazi ya ‘cutter’ kinyume na maoni ya wengi sio kungoa nyasi bali ni kuzitengeneza zipate mwonekano tofauti wa kupendeza.

Akisema ‘cutter’ ina ugumu wa kipekee unaoweza kustahimili dhoruba ya mawe yanayoweza kuharibu kifaa chenyewe

“Faida ya masine yenyewe ni kuwa haiwezi kuvunjika hata ikumbane na shinikizo gani,”alieleza.

Ncha zake huwa zimejificha ndani ya aina fulani ya vyuma vinavyosaidia kusogeza mawe, yanayoweza kuwa kizingiti.

Una mfumo wa masine ndogondogo zinazoshirikiana kuzungusha ncha kali za meno zinazotumika kukata nyasi.

Nicholas anawashauri wakulima wadogo kujipatia mtambo wa cutter,ambao huzingatia kiwango kikubwa cha usafi kwa lishe za mifugo.

Hili litasaidia kupunguza mkurupuko wa maradhi ya mifugo,kama vile Kimeta, Brucellosis na maradhi ya midomo na miguu.