Habari

HILLARY MUTYAMBAI: Tajriba pana ya ujasusi

March 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na BENSON MATHEKA

BW Hillary Nzioki Mutyambai aliyeteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kumrithi Joseph Boinnet kama Inspekta Jenerali wa Polisi ana tajiriba pana katika masuala ya usalama na ujasusi.

Ni tajiriba hii ambayo ilimfanya Rais Kenyatta kuamua kumtwika jukumu la kusimamia usalama wa zaidi ya Wakenya zaidi ya milioni 45.

Hadi uteuzi wake, Bw Mutyambai alikuwa naibu mkurugenzi katika shirika la kitaifa la ujasusi akisimamia masuala ya kukabiliana na ugaidi.

Akiwa katika wadhifa huo, mashambulizi ya kigaidi yalipungua kufuatia habari za kijasusi zilizowezesha polisi kuchukua hatua mapema kuyazima

Bw Mutyambai alijiunga na kikosi cha polisi 1991 na kupanda cheo hadi Superitenda kabla ya kujiunga na shirika la ujasusi 1998.

Katika shirika hilo, aliendelea kupanda cheo na kuwa naibu mkurugenzi wa kushughulikia masuala ya kukabiliana na ugaidi.

Majukumu yake katika cheo hicho yalikuwa ni kuhakikisha nchi ni salama kutoka kwa vitendo vya kigaidi. Aliimarisha ushirikiano wa shirika hilo, polisi na jeshi katika kupigana na ufisadi.

Bw Mutyambai alisomea Chuo Kikuu cha Nairobi kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia ambapo alipata digrii ya uzamili katika masuala ya Sera ya Usalama wa Taifa.

Ni katika chuo hicho ambapo mtangulizi wake katika wadhifa wake mpya Joseph Boinnet alipata digrii yake ya uzamili.

Bw Mutyambai ana tajiriba pana katika masuala ya usalama akiwa alipata mafunzo maalumu ya kukabiliana na ugaidi nchini Amerika, Uingereza na Israel.

Kati ya mwaka 2000 na 2004 alihudumu katika ubalozi wa Kenya Uganda. Mtangulizi wake Boinnet pia alikuwa katika shirika la ujasusi kabla ya kuteuliwa kusimamia polisi.

Aidha, Boinnet aliwahi kuhudumu katika ubalozi wa nchini Zimbabwe na Italia.

Mutyambai atapigwa msasa na Kamati ya Bunge kuhusu Usalama na iwapo ataidhinishwa na bunge atateuliwa rasmi kuwa Inspekta Jenerali wa tatu wa Kenya kusimamia zaidi ya maafisa 100,000 wa polisi.