AKILIMALI: Anawiri katika kilimo baada ya kusaka ajira bila mafanikio
Hata hivyo, wazo hilo likawa kinaya kabisa na aliyotarajia.
Daniel Kihara Nduta anasimulia kuwa alichapa kiguu na njia kwa muda wa mwaka mmoja na nusu katika afisi mbalimbali jijini Nairobi na Kiambu, kutafuta angaa sehemu ya kujishikilia azimbue riziki.
Ni muhimu kutaja katika safari zote hizo aligharamika na mzigo huo ulielekezewa wazazi wake.
“Kila wiki lazima ningeandaa na kupiga chapa wasifu wangu, vyeti vya masomo na barua za kuomba nafasi ya kazi kampuni na mashirika mbalimbali,” asema Kihara.
Isitoshe, pia kulikuwa na nauli ya kusafiri na isiyotabirika Nairobi.
Wasemavyo wahenga; kila mwenda kisimani mapema ndiye huteka maji maenge, licha ya ukakamavu wa kijana huyu kuraukia shughuli hizo alfajiri na mapema, aliteka ‘hewa’.
“Mwaka mmoja na nusu baadaye, sikupokea majibu ya maombi ya kazi wala mwaliko wowote wa kupigwa msasa,” adokeza.
Mtaji
Kila mwaka nchini Kenya katika vyuo vikuu, vyuo anuwai na taasisi za elimu ya juu, maelfu ya vijana hufuzu kwa vyeti mbalimbali, na ni wachache mno wanaopata nafasi finyu za ajira za ofisi.
Bw Kihara anasema mwaka wa 2017, alipoona jitihada zake zimegonga mwamba hakuwa na budi ila kujiunga na orodha ya wanaoweka vyeti vyao vya masomo sandukuni na kutafuta njia mbadala kusukuma gurudumu la maisha.
Barobaro huyu mzawa wa kaunti ya Kiambu anasema amelelewa katika familia ya kilimo, hivyo basi hakijampiga chenga.
Kuzaa si kazi kulea ndiyo kazi, wazazi wake hawakuchoka kuona mvulana wao amepata msingi bora, dhabiti na kujiimarisha kimaisha.
Mwaka huohuo wa 2017, alionyesha mapenzi yake kufanya ufugaji na walimpiga jeki kwa Sh100,000 kuanza safari.
“Zizi la mifugo lilikuwepo, hivyo Sh85,000 za mtaji huo nilizitumia kununua ng’ombe wa maziwa aina ya Friesian na zilizosalia zikawa za kumtunza dhidi ya magonjwa na vimelea,” afichua.
Kihara alikuwa na bahati kama mtende kwa kuwa ng’ombe huyo alikuwa mjamzito, aliyesalia miezi miwili pekee kujifungua.
Anasema alizalisha maziwa kati ya kilo 8-10 kwa siku, kilo moja akiiuza Sh36. Chanda chema huvishwa pete, wazazi walipoona juhudi zake zinavyozaa matunda walimgawia ekari moja na nusu ya shamba ajiimarishe.
Mazao
Anasema ujuzi na maarifa ya ICT aliyopokea chuoni, aliyatumia kufanya tafiti katika mitandao kujua mimea rahisi kupanda na yenye mazao bora na soko la haraka.
“Niligawanya shamba nililopewa nikaanza kulima mboga aina ya Brocolli kwenye thumni ekari (1/8), kabichi (1/8), cornflower (1/8) na mamumunya (1/2) (courgettes). Mamumunya huchukua chini ya siku 45 pekee baada ya upanzi kuanza kuvunwa na yana soko la haraka,” afafanua.
Anaongeza kusema kuwa alitenga 1/2 ekari iwe ya kukuzia ng’ombe nyasi za Napier ya kijani.
Kilimo kilimkubali na kunoga akaongeza ng’ombe mmoja zaidi wa maziwa.
Mwanazaraa huyu pia amekumbatia mfumo wa kukausha nyasi, ‘hay’, akisema mbali na kutunza ng’ombe kitaalamu, huzalisha maziwa mengi wakilishwa majani yaliyokauka.
Utangulizi hata hivyo, haukukosa milima na mabonde, anadokeza kwamba mawakala walimhangaisha kabla kupata soko la moja kwa moja la mazao yake kwa wateja.
Katika kaunti ndogo ya Lari, wadi ya Nyanduma kijiji cha Nduriri, Kiambu ndiko Kihara, 32, anaendeshea shughuli hii ya kilimo na ufugaji.
Unapozuru eneo hilo, mazingira yanayokukaribisha ni ya rangi ya kijani ya majani chai.
Hata hivyo, kijana huyu ameenda kinyume na mkondo wa wakulima wengi, amepamba shamba lake kwa mimea inayochukua muda usiozidi miezi mitatu pekee kuanza kuvunwa.
“Majani chai ukiyapanda mazao ya kwanza utayavuna baada ya miaka minne, kutia msumari moto kwenye kidonda kinachouguza soko lake ni la atiati. Kwa nini nijifunge na kilimo cha aina hiyo, ilhali kuna mazao ya pesa za haraka?” anahoji.
Licha ya kiangazi kinachoendelea kushuhudiwa nchini, shamba la mkulima huyu limesalia na rangi ya kijani. Aidha, ameligawanya kiasi kwamba kila mwezi hakosi kufanya mauzo.
Wakati wa mahojiano alisema licha ya mfumko wa bei ya mazao ya kilimo, akipiga hesabu ya mapato ya kilimomseto chake kila mwezi hakosi kutia kibindoni faida isiyopungua Sh50,000.
Faida ni pato baada ya kuondoa gharama ya matumizi. Ingawa anasema msimu wa mvua kubwa, barabara za eneo la Lari hazipitiki kwa sababu ya ubovu wake, changamoto hii ikimlazimu kuuza mazao kwa bei duni.
“Ombi langu kwa Rais Uhuru Kenyatta wakati akiendelea kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, miundomsingi kama barabara Lari inatatiza jitihada za wakulima, atukumbuke.
Kusafirisha mazao wakati wa mvua ni balaa,” anamhimiza kiongozi wa taifa.