• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
AKILIMALI: Mmoja wa walioitikia wito kukuza parachichi

AKILIMALI: Mmoja wa walioitikia wito kukuza parachichi

Na CHRIS ADUNGO

INGAWA kilimo cha parachichi kinafanywa na wakulima wadogo wadogo wa hapa nchini, kuna pengo kubwa katika juhudi za kufanikisha soko la mazao haya kimataifa.

Katika viwanda, parachichi hutumiwa kutoa mafuta ya upishi na pia bidhaa nyingine za kutengenezea dawa za kila sampuli.

Katika kijiji cha Nyangati, eneo la Mwea katika Kaunti ya Kirinyaga, mkulima Judy Warware Kamanga anasema kwamba amekuwa akijishughulisha na kilimo cha parachichi na maembe kutoka mwaka wa 2002.

Kwa kawaida, mparachichi huchukua muda wa miaka mitatu kabla ya kukomaa na kuanza kutoa mazao.

Bi Warware alianza kwa kupanda mbegu katika kipande maalumu shambani mwake.

Baada ya miezi miwili, miche 12 ikawa imefaulu kuota na hapo akaihamisha na kuipanda katika sehemu nyinginezo za shamba lake kubwa.

Aliipanda miche hii katika mashimo aliyoyachimba hadi kufikia urefu wa futi moja na upana wa futi mbili.

Kisha katika siku za mwanzo mwanzo alihakikisha kuwa ananyunyizia mimea maji mara kwa mara.

Siku zilizofuata, Bi Warware alihakikisha kuwa amepalilia mimea yake ili kupunguza ushindani mkubwa wa kupata maji na madini muhimu kutokana na magugu.

Dawa

Kulingana naye, alihitajika pia kunyunyuzia dawa za kuzuia wadudu hatari.

Katika mwaka wa 2010 alipata mavuno kwa mara ya kwanza, ijapokuwa si kwa wingi.

Lakini miaka iliyofuata, mavuno yaliongezeka maradufu.

Kila mwaka, yeye huvuna parachichi kati ya Februari hadi Juni na kuwauzia wafanyabiashara wadogo wadogo au baadhi ya kampuni zinazouza parachichi au bidhaa kutokana na zao hili katika nchi za kigeni.

Miparachichi anayoipanda ni aina ya Kent na anapovuna, mparachichi mmoja huweza kumtolea zaidi ya maparachichi 1,000 katika msimu mzima wa mavuno.

Na kwa hivyo, katika msimu wa mavuno wa muda wa miezi minne hivi, ana uwezo wa kupata maparachichi zaidi ya 12,000.

Anapouza mazao yake, parachichi moja hunadiwa kwa kati ya shilingi tano hadi Sh10 kulingana na ukubwa wa tunda au hali ya soko ilivyo.

Anasema mparachichi mmoja una uwezo wa kutoa mazao mengi kadri mti unavyozidi kukomaa.

Kulingana na Bi Warware, kilimo cha parachchi kina faida na huwa kinamwezesha kupata riziki ya kila siku kwani shughuli za kilimo kwake ni sawa na ajira rasmi.

Zaidi, amewezeza pia kuwasomesha wanawe watatu kupitia kwa mapato yanayotokana na kilimo cha parachichi.

Anaeleza kuwa kilimo cha parachichi hakihitaji muda mwingi wa kuwa shambani kwani mmea unapokomaa, mkulima huhitajika tu kupalilia na kutilia dawa mimea yake ili kuitunza ipasavyo.

Baadhi ya changamoto anazokumbana nazo ni pamoja na bei ya chini ya parachichi anapowauzia wafanyabiashara wadogowadogo ambao hununua kwa bei ya chini ilhali wanapofikisha mazao haya sokoni, hupata faida kubwa kwa kuwauzia wateja kwa bei ghali zaidi.

Mbali na magonjwa ya kila sampuli hasa yanayotokana na kiangazi au baridi kali kupita kiasi, changamoto nyingine ni mvua ya mawe inayoharibu matunda au kuoza kwa maparachichi iwapo soko litakosekana baada ya zao kukomaa shambani.

Ushauri wake ni pawepo na mipango maalum kutoka kwa serikali ya Kaunti ya Kirinyaga, ya kutafuta masoko ya kigeni ili wakulima wa parachichi wafaidike zaidi.

“Wakulima wengi wa parachichi hawana ujuzi mwingi wa teknolojia ya kisasa inayohitajika kuboresha au kuongeza mazao yao. Hivyo basi, litakuwa jambo la busara kwa wakulima kuelimishwa na maafisa wa kilimo wa serikali,” Bi Warware anasema.

Mnamo 2012, aliboresha mradi wake akaanza kupandikiza (grafting) na hatimaye akazalisha aina ya avokado za kisasa ambazo ni chotara (Hass) kwa mtaji uliogharimu hadi Sh15,000.

Mavuno yake yanapokuwa tayari, huhifadhiwa vizuri katika eneo lenye joto kiasi na sehemu isiyokuwa na unyevu.

Kulingana na muda, mkulima atafahamu kuwa maparachichi yamekuwa mabivu na tayari kuliwa iwapo mazao yataanza kubadilisha rangi na unapotomasa tunda bivu au lililoiva, hubonyea.

Kinyume na maparachichi ya kawaida, mche mmoja uliopandikizwa unaweza kumpatia Bi Warware kati ya matunda 300-500 kwa msimu mmoja.

Uwezo wa kuzaliwa kwa matunda huongezeka kadri muda unavyokuwa.

Miche kukomaa

Miche inapotimu umri wa miaka mitano, huwa imekomaa na mkulima anaweza kupata hadi parachichi 1,500 kila mwaka.
Katika gunia moja lililoshonwa vizuri, Bi Warware hupakia kati ya avokado 400-600.

Bei ya maparachichi haya yaliyozaliwa kwa upandikizaji ya Hass ni Sh15 kwa kila tunda.

Inapomlazimu kusafirisha maparachichi yake hadi masoko ya mbali nje ya Kaunti ya Kirinyaga, tunda moja huuzwa kwa hadi Sh25 ili kufidia gharama kubwa ya usafirishaji.

Katika sehemu ya robo ekari ya shamba lake kwa sasa, amepanda mbegu 10,000 ambazo kabla ya kupandwa, alizitibu ili kuzuia magonjwa yanayotokana na mchanga.

Katika shughuli za upanzi, Bi Warware huwa anaajiri wafanyakazi ambao humsaidia kutia mbolea ya mbuzi katika mifuko ya vijikaratasi kisha kuweka mbegu.

Baada ya hapo, kazi huwa ni kunyunyizia maji kila siku na kwa kawaida, miparachichi hii huchukua mwezi mmoja ili kukua.

Kulingana naye, huwa anaanza kupandikiza miche hii baada ya miezi miwili kutoka siku ya upanzi.

Madhumuni ya upandikizi ni kupata aina bora ya maparachichi yatakayowavutia wateja.

Kwa kawaida, ana aina mbili za avokado ambazo ni ‘Hass’ na ‘Fuerte’. Anasema aina hizi mbili ndizo zinahitajika sokoni kwa wingi.

“Lengo hasa la kufanya upandikizi ni kuhakikisha kuwa aina sawa ya maparachichi imepatikana; na zaidi ni kupunguza muda wa parachichi kukua na kukomaa,” anasema.

Katika misimu ya mvua, huwa anauza miche mingi ya miparachichi ikilinganishwa na misimu mingine katika mwaka.

Anasema kwamba kila mwaka ana uwezo wa kuuza hadi miche 10,000 ambapo mche mmoja huuzwa kwa Sh150.

Ina maana kwamba kwa kipindi cha miezi 12, Bi Warware ana uwezo wa kujivunia zaidi ya Sh1.5 milioni.

You can share this post!

DPP Haji atoa orodha ya washukiwa wa ufisadi kutoka...

Mhadhiri wa MKU atuzwa kwa ubunifu wake

adminleo