Michezo

Angaza FC yazidi kung'aa katika ulingo wa soka

March 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO
KLABU ya Angaza FC ni miongoni mwa timu zina makao makuu katika kitongoji cha Kiandutu, Thika, Kaunti ya Kiambu.
Timu hiyo chini ya kocha mpya Evans Okwemba inaboresha talanta za wanasoka chipukizi angalau kuimarisha viwango vya mchezo wao ili kujiweka mstari wa mbele.
Timu hiyo ya vijana chipukizi inajivunia kucheza kwenye mechi ya Aberdare Regional League ambapo ilipangwa kwenye Kundi A na hadi kufikia sasa ina alama name katika nafasi ya tano katika Ligi yenyewe.
Aliyekuwa kocha wa hapo awali, Victor Kabanji, amechukua mikoba ya wadhifa wa meneja wa timu, lengo likiwa ni kuiendesha timu kuwa imara zaidi.

Kocha Okwemba anaeleza kuwa tangu ligi hiyo ing’oe nanga miezi miwili iliyopita wamecheza mechi tano.

Kati ya mechi hizo Angaza imeshinda mbili ikapoteza mbili na kutoka sare mbili.

Hapo awali Angaza iliigonga Kenchic kwa mbao 2-0.

Baadaye waliikomoa Destiny bao 1-0.

Timu hiyo ilitota mbele ya Ngecha kwa mabao 2-0. Nayo Thika Cloth Mills iliwagonga kwa bao 1-0.

Walitoka sare ya 1-1 na Jungle Nuts FC.

Changamoto

Kocha huyo anasema changamoto kubwa anayopitia   ni kukosa hela  za kuwasafirisha vijana wake kwenda kucheza sehemu za mbali.

“Wengi wa chipukizi hawa ni wanafunzi wa shule za upili ambapo wakati fulani kila mmoja huingia mfukoni kuchanga kidogo alicho nacho. Kwa hivyo tunaomba wahisani popote walipo wajitokeze kusaidia timu yetu ya vijana,” alisema Okwemba.

Baadhi ya wachezaji wanaoipa timu hiyo uhai wa kuendelea ni Lawrence Mwangi (golikipa), madifenda Anthony Gitonga, Charles Wanyoike, Samuel Kiringa, na Evans Mathayo.

Kiungo cha kati wapo Hamsick Njoroge, Hamza Rashid, Ben Njoroge,  na John Kimohu. Mastraika ni George Karanja, Ben Njoroge, na David Waweru. Nahodha wa timu ni Samuel Kiringa.

Kwa jumla anazidi kuwahimiza vijana wake  kuzingatia na kudhamini mazoezi ili kuboresha talanta zao katika sekta ya soka.

Anasema timu hiyo hufanya mazoezi yake kutoka Jumanne hadi Ijumaa katika Uwanja wa shule ya upili ya Broadway, Thika.

Anasema kwa sasa wanachokamia kupata ni mdhamini ambaye atajitolea kuinua vijana hao ambao wako gangari kuinua timu.

Anasema eneo la Kiandutu, Athena na Kiganjo lina vijana wengi wazuri wenye vipaji ambao wakipewa mwongozo bila shaka wanaweza kufanya maajabu.