Mamilioni kwa Jepkosgei baada ya kuwika New York City Half Marathon
Na GEOFFREY ANENE
MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya mbio za kilomita 21 Joyciline Jepkosgei amejizolea Sh2,003,600 baada ya kunyakua taji la New York City Half Marathon nchini Marekani, Jumapili.
Jepkosgei ameshinda jijini New York ambako Kenya haikuwa imetwaa taji la kinadada kwa miaka minne mfululizo.
Mkimbiaji huyu mwenye umri wa miaka 25, ambaye anapanga kuanza kushindana katika mbio za kilomita 42 baadaye mwezi ujao, alikata utepe jijini New York kwa saa 1:10:07.
Mkenya mwenzake Mary Ngugi aliridhika katika nafasi ya pili kwa saa 1:11:07. Alijizolea Sh1,001,800 naye bingwa wa mwaka 2018 Buze Diriba kutoka Ethiopia akatia mfukoni Sh550,990 kwa kumaliza katika nafasi ya tatu kwa muda sawa na Ngugi.
Kabla ya ushindi wa Jepkosgei, Kenya iliwahi kutwaa taji la New York Half Marathon kupitia kwa Catherine Ndereba mwaka 2006 na 2008, Hilda Kibet (2007) na Caroline Rotich (2011 na 2013) na alikuwa Sally Kipyego mwaka 2014.
Kwa mwaka wa tatu mfululizo, Kenya iliambulia pakavu katika kitengo cha wanaume cha New York Half Marathon.
Kenya imewahi kushinda taji la wanaume mara saba. Washindi kutoka Kenya ni Tom Nyariki mwaka 2006, Peter Kamais (2010), Peter Kirui (2012), Wilson Kipsang (2013), Geoffrey Mutai (2014), Leonard Korir (2015) na Stephen Sambu (2016).
Jepkosgei anashikilia rekodi ya mbio za kilomita 21 duniani ya saa 1:04:51 ambayo aliweka mjini Valencia nchini Uhispania mwaka 2017.
Alinuia kuingia katika marathon mjini Honolulu nchini Marekani mwezi Desemba mwaka 2018, lakini akajiondoa dakika ya mwisho kwa sababu ya jeraha.
Matokeo ya New York Half Marathon 2019:
Wanawake
Joyciline Jepkosgei (Kenya) saa 1:10:07
Mary Ngugi (Kenya) 1:11:07
Buze Diriba (Ethiopia) 1:11:07
Emma Bates (Marekani) 1:11:13
Desiree Linden (Marekani) 1:11:22
Birtukan Fente Alemu (Ethiopia) 1:12:17
Bevery Ramos (Puerto Rico) 1:12:33
Kellyn Taylor (Marekani) 1:12:43
Samantha Palmer (Marekani) 1:12:52
Lindsay Flanagan (Marekani) 1:13:13
Wanaume
Belay Tilahun (Ethiopia) saa 1:02:10
Daniel Mesfun (Eritrea) 1:02:16
Paul Chelimo (Marekani) 1:02:19
Jared Ward (Marekani) 1:02:33
Noah Droddy (Marekani) 1:02:39
Brogan Austin (Marekani) 1:02:41
Tim Ritchie (Marekani) 1:02:51
John Raneri (Marekani) 1:02:51
Parker Stinson (Marekani) 1:02:55
Ben True (Marekani) 1:02:56