Meltah Kabiria yainyeshea Kawangware 4-0 Super 8
Na JOHN ASHIHUNDU
Kinyume na ilivyotarajiwa, klabu ya Meltah Kabiria iliimiminia Kawangware United mabao 4-0 katika mechi ya Super 8 Premier League iliyochezewa Riruta Stadium, Jumapili.
Nyota wa mechi hiyo, Collins Omondi alipachika wavuni mabao matatu na kuisaidia timu yake kupata ushindi wa kwanza katika mechi mbili, baada ya hapo awali kushindwa 3-1 na Jericho All Stars.
Licha ya matokeo hayo ya kushangaza, timu zote zilicheza mchezo wa kuvutia huku washindi wakijipatia bao la kwanza dakika ya tisa kupitia kwa Omondi.
Kawangware United ambao walikuwa wenyeji katika mechi hiyo walipewa penalti iliyopigwa na John Mureithi, lakini ikaokolewa na kipa Patrick Githiga.
Meltah walijipatia bao la pili dakika chache kabla ya muda wa mapumziko baada ya Omondi kumchanganya kipa katika eneo la hatari.
Huku wakicheza kwa presha tele, mlinzi wa United alicheza vibaya na kusababisha penalti ambayo ilifungwa na Wilson Muhoto.
Omondi alizima kabisa matumaini ya Kawangwre alipomimina wavuni bao la tatu dakika ya 77.
“Ilikuwa mechi nguvu lakini mbinu zetu zilituwezesha kufalu. Nawapongeza mashabiki wetu kwa kushangilia vijana hadi dakika ya mwisho,” alisema kocha wa Kabiria, Urbanus Mwangi.
Kwa upande mwingine, mashabiki wa Kawangware walirejea makwao wakiwa shingo upande kufuatia kichapo hich, hii ikiwa mechi ya pili kupoteza msimu huu.
“Tulishindwa kwa sababu wachezaji wetu wengi wamejiunga na timu nyingine katika ligi mbali mbali. Wachezaji tunaotumia hawajakomaa wala kuzoeana,” alisema kocha Francis Thairu wa Kawangware
Ugani Camp Toyoyo, Jericho All-Stars walitoka nyuma mara mbili kabla ya kuibuka na ushindi wa 3-2 dhidi ya MASA. Wenyeji walipata bao la ushindi kupitia kwa Brian Kasasi dakika ya mwisho b Kelvin Ndung’u kufunga mengine awali katika dakika za 74 na 84.
Ushindi huo umeipeleka Jericho kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, huku wakifuatiwa na Shauri Moyo Sportiff, kwa pointi sawa (sita), lakini tofauti ya mabao. Mabao ya MASA yalipatikana kupitia kwa Alex Oyugi na Patrick Aura.
Kwingineko, TUK FC walipata ushindi finyu wa 1-0 dhidi ya Team Umeme kwenye mechi iliyochezewa Kabete Cavs. Bao hilo muhimu liliupachikwa wavuni na Joseph, dakika ya 79.
Katika uwanja wa Makongeni, timu geni ya Shauri Moyo Sportiff iliandikisha ushindi wa pili kwa kuinyuka NYSA 1-0 lililofungwa na Moses Bara.
Matokeo ya mechi za wikendi kwa ufupi yalikuwa:
Huruma Kona 0-0 Metro Sports
Shauri Moyo Sportiff 1-0 NYSA
Meltah Kabiria 4-0 Kawangware United
TUK 1-0 Team Umeme
Makadara Junior League SA 1-2 Githurai All Stars
Rongai All Stars 1-1 Lebanon FC
Mathare Flames 2-1 Dagoretti Former Players FC