Sh10 milioni kwa Kiplagat baada ya kushinda Seoul Marathon
Na GEOFFREY ANENE
MKENYA Thomas Kiplagat alijizolea jumla ya Sh10 milioni baada ya kushinda Seoul Marathon nchini Korea Kusini mnamo Machi 17, 2019.
Mkimbiaji huyu alijishindia Sh kujizolea Sh8,056,800 tuzo ya washindi na kuongezwa Sh2,014,200 kwa kumaliza umbali huo wa kilomita 42 kati ya saa 2:06:00 na 2:06:59.
Alikata utepe kwa saa 2:06:00 akikosa Sh3,021,000 kwa sekunde moja. Angeshinda Seoul Marathon kwa kati ya saa 2:05:37 na 2:05:59, angeongezwa bonasi ya Sh5,035,000. Ushindi wa Kiplagat uliendeleza utawala wa Kenya katika kitengo cha wanaume hadi miaka mitano baada ya Wilson Loyanae kunyakua mataji ya mwaka 2015, 2016 na 2018 naye Amos Kipruto akabeba taji la mwaka 2017.
Katika makala haya ya 75, Kiplagat alinyoa karibu dakika mbili kutoka muda wake bora wa saa 2:07:52 alioweka akishinda Joongang Marathon mwaka 2014.
Alifuatwa kwa karibu na Mkenya mwenzake Elisha Kipchirchir Rotich (2:06:12), ambaye pia aliimarisha muda wake kutoka 2:07:32 alioweka akitwaa ubingwa wa Eindhoven Marathon mwaka 2018.
Mike Kiptum Boit pia kutoka Kenya alikamilisha orodha ya wakimbiaji watatu wa kwanza baada ya kutimka 2:06:24. Rotich na Boit walizawadiwa Sh4,024,400 na Sh2,012,200, mtawalia.
Kwa mwaka wa pili mfululizo, Kenya iliambulia pakavu katika kitengo cha kinadada, huku mwanariadha wake wa kwanza kuvuka mstari wa kimalizia mbio akiwa Celestine Chepchirchir katika nafasi ya tatu.
Mbahraini Desi Jisa Mokonin alinyakua taji kwa saa 2:23:45 akifuatwa na Muethiopia Hirut Tibebu Damte (2:24:10). Chepchirchir alimaliza kwa saa 2:24:49. Mokonin alizawadiwa Sh8, 056, 800 na kuongezwa bonasi ya Sh1,006,100 kwa kutimka kati ya saa 2:22:00 na 2:23:59.
Washikilizi wa rekodi za Seoul Marathon ni Loyanae aliyeshinda taji la wanaume mwaka 2016 kwa saa 2:05:13 na Mchina Zhou Chunxia aliyenyakua taji la wanawake kwa saa 2:19:51 mwaka 2006.
Matokeo ya Seoul Marathon mwaka 2019:
Wanaume
Thomas Kiplagat Rono (Kenya) saa 2:06:00
Elisha Kipchirchir Rotich (Kenya) 2:06:12
Mike Kiptum Boit (Kenya) 2:06:24
Fikre Bekele Tefera (Ethiopia) 2:06:27
Robert Kiplimo Kipkemboi (Kenya) 2:07:11
Tsegeye Kebede (Ethiopia) 2:09:06
Sammy Kitwara (Kenya) 2:09:52
Wanawake
Desi Jisa Mokonin (Bahrain) saa 2:23:45
Hirut Tibebu Damte (Ethiopia) 2:24:10
Celestine Chepchirchir (Kenya) 2:24:49
Zinash Mekonen Lema (Ethiopia) 2:25:44
Mercy Jerotich Kibarus (Kenya) 2:27:20
Ahn Seul-Ki (Korea) 2:26:28
Merima Mohamed (Bahrain) 2:27:34