• Nairobi
  • Last Updated March 19th, 2024 1:13 PM
Everton wacharaza Chelsea na kuweka Sarri padogo Stamford

Everton wacharaza Chelsea na kuweka Sarri padogo Stamford

Na MASHIRIKA

LONDON, UINGEREZA

MATUMAINI ya Chelsea ya kumaliza kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ndani ya mduara wa nne-bora jedwalini msimu huu yalididimizwa zaidi wikendi jana.

Hii ni baada ya masogora hao wa kocha Maurizio Sarri kupokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Everton ugani Goodison Park.

Ni matokeo ambayo kwa mujibu wa wachanganuzi wa soka, yananing’iniza pembamba mustakabali wa Sarri uwanjani Stamford Bridge.

Kwingineko, Manchester City walidumisha uhai wa tumaini la kutia kapuni jumla ya mataji manne msimu huu baada ya kupangwa na Brighton katika nusu-fainali za Kombe la FA.

Nusu-fainali nyingine ya droo hiyo itawakutanisha Watford na Wolves ugani Wembley kati ya Aprili 6-7.

Man-City walifuzu kwa hatua ya nne-bora ya Kombe la FA baada ya kutoka nyuma na kuwacharaza Swansea City 3-2 uwanjani Liberty huku Brighton wakiwabandua Millwall kupitia mikwaju ya penalti.

Watford ambao walitinga fainali ya Kombe la FA mnamo 1984, watakuwa wakishiriki nusu-fainali yao ya kwanza ya kipute hicho tangu mwaka 1998.

Licha ya Chelsea kutamalaki kipindi kizima cha kwanza na kumiliki asilimia kubwa ya mpira, mabingwa hao wa 2016-17 walipoteza nafasi nyingi za wazi.

Mkwaju wagonga mwamba

Eden Hazard alishuhudia mkwaju wake ukigonga mwamba kabla ya Pedro Rodriguez kuipaisha fataki hata baada ya kusalia peke yake na kipa Jordan Pickford.

Utepetevu huo wa Chelsea uliwaweka katika nafasi ya kuadhibiwa na Everton waliojipa uongozi kupitia kwa Richarlson Andrade dakika nne baada ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa kipenga cha pili kupulizwa.

Bao la Richarlson lilikuwa lake la 13 katika kampeni zote za msimu huu ndani ya jezi za Everton.

Masaibu ya Chelsea yalizidishwa na Gylfi Sigurdsson aliyefunga mkwaju wa penalti kunako dakika ya 71 baada ya Marcos Alonso kumchezea Richarlson visivyo ndani ya msambamba.

Matokeo hayo yanawasaza Chelsea katika nafasi ya sita kwa alama 57, moja nyuma ya Manchester United ambao wangalisalia nyuma yao iwapo wangetia kapuni alama tatu.

Ushindi pia ungaliwapaisha Chelsea hadi nafasi ya tano kwa alama sawa na Arsenal ambao kwa sasa wanafunga mduara wa nne-bora kwa pointi 60.

Awali, Liverpool walirejea kileleni mwa jedwali kwa alama 76 baada ya kuwachabanga Fulham 2-1 uwanjani Craven Cottage na kuwaruka mabingwa watetezi Manchester City ambao kwa sasa wanajivunia alama 74.

Kwa mujibu wa Sarri, kichapo kutoka kwa Everton kilidhihirisha sifa za ukosefu wa uthabiti, moyo wa kujituma na kiu ya mafanikio miongoni mwa wachezaji wake.

Baada ya matumaini ya kutinga nne-bora kuyumbishwa, Chelsea kwa sasa wanasalia na ulazima wa kutia kapuni ubingwa wa Ligi ya Uropa ili kujikatia tiketi ya kushiriki kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Ushindi wa Everton ambao kwa sasa wananolewa na kocha Marco Silva ulikuwa wao wa kwanza tangu Januari 2017 dhidi ya vikosi vinavyofunga orodha ya sita-bora kwenye jedwali la EPL.

Mchuano huo ulikuwa wa nne kati ya mitano iliyopita kwa Chelsea kupoteza ugenini katika EPL.

Ni Fulham pekee ndio wanaojivunia rekodi duni zaidi ya hiyo ya Chelsea ambao huenda wakalazimika kumtimua Sarri iwapo hatawajinyanyua na kujikweza pazuri jedwalini mwishoni mwa msimu huu.

Kwa mujibu wa Chris Waddle ambaye ni winga wa zamani wa Tottenham na timu ya taifa ya Uingereza, Sarri atajilaumu mwenyewe iwapo atatimuliwa Chelsea.

Kulingana na mchanganuzi huyo wa soka, Sarri angalikuwa pema zaidi iwapo angalimwajibisha vilivyo mvamizi Olivier Giroud ambaye anajivunia fomu nzuri badala ya mkongwe Gonzalo Higuain.

You can share this post!

Messi afungia Barcelona ‘hat trick’ ya 33 La...

MAPISHI: Wali wa nazi na nyama iliyosagwa

adminleo