• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Niko radhi kuacha Chelsea lakini si sigara, adai Sarri

Niko radhi kuacha Chelsea lakini si sigara, adai Sarri

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA Maurizio Sarri wa Chelsea amesema anaweza kuacha kuinoa Chelsea, lakini sio uvutaji wa sigara.

Tabia ya mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 60, imewashinda mashabiki wa klabu hiyo ambao wameanza kudhania huenda tabia yake ya uvutaji sigara kwa wingi inamfanya asiwe mfano mzuri kwa wachezaji wake.

Tofauti na Italia, Uingereza ina sheria kali dhidi ya uvutaji sigara hadharani na maeneo mbalimbali ikiwemo viwanja vya michezo, hivyo inakuwa vigumu kwa kocha huyo kuvuta akiwa uwanjani.

Sarri ni kati ya makocha maarufu wenye tabia ya uvutaji sigara kupita kiasi, na kwa wakati mwingi amekuwa akitoka haraka na kuingia vyumba maalum kuvuta pafu kadhaa na kurejea kuendelea kutoa mawaidha wakati wa mapumziko.

Pamoja na tabia hiyo, Sarri amekuwa akiwaambia wachezaji wake kutoiga tabia yake kwani inaweza kuwaletea shida katika kazi yao ya uchezaji.

Kocha Maurizio Sarri wa klabu ya Chelsea. Picha/ AFP

Sarri amekuwa akiwaambia mashabiki na waandishi kwamba sio rahisi kuacha kuvuta sigara kutokana na ukweli sigara ndani yake ina kemikali inayofanya mtu awe na uraibu, hivyo kumfanya atamani kuitumia kila mara.

Kupumbaza akili

Imebidi Sarri aanze kutumia sigara ya kielekroniki kudanganya akili yake. Sigara hii ina kichungi, umbo, harufu ya moto kama sigara lakini haitoi moshi.

Mtu anapoivuta anahisi kama anavuta sigara ya kweli, kumbe ni bandia.

Hali hii pia inatumika kumfanya mtu akabiliane na uvutaji wa kupindukia.

Hali nyingine ya kuachana na sigara ni kuepuka makundi au marafiki wanaomshawishi mtu atumie tumbaku. Pia ni bora kwenda sehemu ambazo zimekataza matumizi ya sigara.

Kadhalika mtu anaweza kuepuka kuvuta kwa kupendelea kutumia chakula ambacho kinaondoa hamu ya kuvuta.

Wengine nao hutembelea sehemu za kutoa huduma za afya kwa ushauri, lakini kwa Sarri, ni rahisi kuachana na Chelsea lakini sio sigara.

Huenda kocha huyo akatimuliwa baada ya Chelsea kuendelea kupoteza matumaini ya kumaliza ligi miongoni mwa nne za kwanza.

Everton yaicharaza Chelsea

Miamba hao, walipokea kichapo cha 2-0 kutoka kwa Everton ugani Goodison Park, matokeo ambayo yanafanya uwezo wa kocha huyo kuendelea kuwa Stamford Bridge kuwa mdogo.

Timu hiyo, tayari imeondolewa katika mashindano ya FA Cup na League Cup.

Chelsea walimiliki kwa kipindi kikubwa mchezo wao dhidi ya Everton lakini wakashindwa kufunga mabao ya kuwapa ushindi.
Kwa sasa, wanashikilia nafasi ya sita kwa alama 57, moja nyuma ya Manchester United ambao wangekuwa nyuma yao iwapo wangeibuka na ushindi dhidi ya Everton.

Kadhalika, ushindi ungewaweka katika nafasi moja na Arsenal wanaofunga orodha ya nne bora.

You can share this post!

5 kutochezea Gor katika kipute cha nane-bora kimataifa

MASAIBU: Staa mashakani kwa kukejeli kocha

adminleo