• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 10:08 PM
AKILIMALI: Maua kama mbinu ya kukabiliana na wadudu waharibifu shambani

AKILIMALI: Maua kama mbinu ya kukabiliana na wadudu waharibifu shambani

Na GRACE KARANJA

KILIMO hai au kuvuna mazao yatokanayo na kilimo kinachoepuka dawa zilizotengenezwa viwandani, huenda wakati mwingine ikawa ni changamoto kubwa hasa kwa wakulima walio na ekari nyingi za mashamba.

Ikizingatiwa kuwa wateja wa mazao haya ambao ndio walaji, mwanzo wanafanya utafiti ili kufahamu vyema ikiwa wakulima wanazingatia kilimo hai kama wengi wanavyosema, kwa sababu mazao mengi huwa sio salama katika mwili wa mwanadamu.

Hata hivyo, wataalamu wanasema kwamba ili kubadilisha shamba lako kutoka kilimo cha kisasa na kukifanya kilimo hai itachukua muda wa miaka mitatu kabla ya kuvuna mazao ya kwanza yatakayothibitishwa kuwa bila kemikali yoyote.

Kufanya kilimo biashara katika udongo ulio na afya kunajumuisha upendo wa shamba lililorutubishwa kwa kutumia mbolea za kiasili, lakini wakati wadudu waharibifu wanapovamia shamba na kuharibu bidii ya mkulima kwa kula mazao yake linalomjia mkulima kwenye fikra zake ni kukimbia na kununua madawa ya kuua wadudu, kuyachanganya, na papo hapo kuanza kuyanyunyizia mimea.

Paul Kagoni, afisa msaidizi wa mauzo ya mbegu katika Kampuni ya Starke Ayres tawi la Kaunti ya Nairobi akionyesha maua aina ya Marigold yaliyopandwa kandokando ya mimea ya mamumunya ili kuvutia wadudu badala ya kuharibu mazao. Picha / Grace Karanja

Shughuli hii inaweza kutia kemikali mbaya kwenye kitovu chako cha maji kwa sababu ni adui kwa mazingira, na kwa wakati mmoja kuharibu udongo.

Kwa muda mrefu michanganyiko ya mafuta na maji, sabuni na maji, kitunguu saumu, pamoja na pili pili kali ni njia mojawapo ambayo imekuwa ikitumika kunyunyizia mimea na wakulima hii ikiwa ni kujumuisha kilimo hai na kulingana na wao imekuwa yenye faida na gharama yake ni nafuu.

Wakati wa mahojiano kwa simu, licha ya mchanganyiko huu kutumika kama dawa za kuzuia wadudu waharibifu mtaalamu Samuel Gacheru ambaye ni afisa wa mauzo ya mbegu kutoka Kampuni ya Starke Ayres tawi la Kaunti ya Nairobi, anaeleza kwamba kando na kurembesha shamba la mkulima, maua pia yanaweza kutumika kama njia ya kuwafurusha na hata kuwaua wadudu waharibifu na yanaweza kupandwa shambani badala ya kunyunyizia mimea madawa ya kemikali.

“Maua aina ya Marigold hupandwa shambani pamoja na mimea ya mboga kama vile kabeji, nyanya, matango na mamumunya.

Wakati wadudu waharibifu wanapokuja kuharibu mazao, maua haya wakati yanachanua hutoa harufu isiyo ya kupendeza hivyo hufukuza inzi weupe, kuua viwavi wabaya na kwa wakati mmoja yanaweza kuwaua sungura wa mwitu,”anaeleza Bw Gacheru.

Hata hivyo, Bw Gacheru anasema kuwa sio wadudu wote wanaokuja shambani ambao ni waharibifu.

Buibui na vunjanjugu hufuata na kula wadudu wadogowadogo ambao mkulima hawezi kuwaona kwa macho.

Anasema kuwa kunyunyizia madawa ya kemikali shambani huwaua wasaidizi hawa.

“Wengine kama vile vipepeo na nyuki hupendezwa na shamba lililopandwa maua na punde wanapoanza kunyonya wanasaidia katika shughuli ya uchavushaji hivyo kuongeza mazao ya mimea kwa wakulima,” anaendelea kueleza Bw Gacheru.

Mtaalamu Samuel anasisitiza kwamba wakulima wawe na uzoefu wa kuchanganya maua katika shamba la mboga ingawa sio rahisi ili kupunguza gharama ya ununuzi wa madawa ya kemikali.

You can share this post!

AKILIMALI: Mtambo wa kuangua mayai umeimarisha idadi ya kuku

AKILIMALI: Ajikimu kimaisha kwa kuchora na kuchonga vibonzo

adminleo