Makala

AKILIMALI: Ajikimu kimaisha kwa kuchora na kuchonga vibonzo

March 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LUDOVICK MBOGHOLI

JOHN Solly Savala amekuwa na ujuzi wa pekee miongoni mwa wafanyabiashara wachache mjini Mombasa, kwa umaarufu wa biashara ya kuuza vibonzo anavyochora na kuchonga nyumbani kwake mjini Mazeras.

Akihojiwa na Akilimali, Savala anasema alizaliwa na kipaji cha uchoraji na uchongaji vibonzo kabla ya kutumia kipaji hicho kibiashara.

“Ninabuni michoro na kuichongea sanamu nikitumia vifaa visivyonigharimu kifedha na kuvisaga kabla ya kuvichanganya kuboresha kazi yangu,” anasimulia Mzee Savala.

Savala anasema anazingatia mno uchoraji wa viumbe wa baharini mbali na viumbe wa nchi kavu kama hatua ya kuwavutia wateja katika maeneo ya bara na pwani kwa jumla.

Chimbuko la biashara yake ni mtalii aliyemtembelea mwaka 2004 kutoka Austria ambaye alipendezwa na kazi yake.

“Mtalii huyo alinijia akitaka kunisaidia zaidi kibiashara, akanipa motisha ya kujiendeleza,” asema.

Aeleza kuwa alikuwa mtalii mwanamke kutoka shirika la Fortuna Media Arts Gallery lenye makao yake Vienna huko Austria.

“Alinichukua picha ya video nikiboresha michoro na kuchonga sanamu.”

Michoro ya Savala tayari imevutia mataifa ya Ujerumani, Marekani, Uingereza na Italia mbali na shirika la makavazi nchini. Shirika la MASKPRIZE kutoka Uingereza lilimpa tuzo ya ‘mwalimu bora wa ubunifu wa sanaa’.

Kuhusu soko la bidhaa zake, Savala anasema hujitahidi kufikia upeo wa juu zaidi kibiashara kwasababu ni watu wachache wa rika lake wanaojishughulisha na kazi hii’.

Hata hivyo, anasema mapato mazuri ya kazi yake hutegemea ubora wa michoro.

Biashara ya John Solly Savala inaenda na msimu kwani kuna misimu ambayo bei ya bidhaa zake ni ghali zaidi huku misimu mingine bei ikishuka na kumtatiza kimapato.

Anasema miaka michache iliyopita biashara yake ilididimia kwa ukosefu wa wateja.

Msimu wa mapato mazuri picha moja ya mchoro wa urefu wa futi moja inampatia kati ya takriban Sh4,000 na Sh5,000, huku msimu usiokuwa na mapato picha hiyo inampatia kati ya Sh2,500 na Sh3,000.

Picha kubwa

Hata hivyo, biashara yake hunawirishwa kimapato na michoro ya picha kubwa zenye urefu wa futi sita hadi saba na upana wa kuanzia futi nne hadi tano na saba.

Anasema mauzo ya picha hizo yanampa pato la kati ya Sh7,000 hadi 10,000 kwa picha moja.

“Kidogo navuna mapato mazuri kwa michoro ya picha hizo, lakini hasara yake pia ni kubwa kwasababu nisipouza utendakazi wangu hauna manufaa yoyote,” asema akidokeza kuwa uchongaji wa sanamu ndio wenye kumpatia manufaa makubwa endapo anajiwa na wateja wanaohitaji kazi yake.

Alianza biashara ya michoro na uchongaji zaidi ya miaka 30 iliyopita kabla hajaoa na alipooa ndipo aliongeza bidii na ujuzi zaidi ili aweze kuitimizia familia yake mahitaji ya kimsingi.

Savala anaambia Akilimali mara tu baada ya kuwa na familia, ubunifu wake uliongezeka huku akitafuta vifaa visivyomgharimu pesa nyingi.

Biashara yake imekuwa tegemeo kwani inamwezesha kukimu mahitaji ya familia.