SHANGAZI AKUJIBU: Nilimuacha kwa tabia mbaya, sasa ataka kurudi
Na SHANGAZI
VIPI Shangazi? Nimeachana na mpenzi wangu baada yake kubadilisha ghafla mienendo yake. Tulipoanza uhusiano wetu, mpenzi wangu alikuwa mwanamke mwenye heshima sana kwangu, lakini wakati fulani alibadilika akaanza kunionyesha madharau na ikabidi nimuache. Sasa anataka turudiane lakini mimi simtaki ninatafuta mwingine. Ninaomba ushauri wako.
Kupitia SMS
Ni muhimu kwa mtu kuwa na msimamo maishani. Kama una hakika kuwa huwezi kurudiana na mpenzi wako huyo na unashughulika kutafuta mwingine, sielewi ni kwa nini unataka ushauri wangu. Tenda kulingana na uamuzi wako.
Mume anashindwa kulima hadi nihisi kafikishwa patamu!
Shangazi hujambo? Nimeolewa kwa muda sasa na nina tatizo. Tangu tuoane mwenzangu hajawahi kunitosheleza kwa huduma za chumbani. Tumejadili suala hilo mara kadhaa na amekuwa akisingizia kuchoka kutokana na kazi zake ofisini. Nifanyeje?
Kupitia SMS
Ndoa ina changamoto nyingi na hiyo ni mojawapo. Subira na uvumilivu zinahitajika katika kudumisha mapenzi na ndoa. Usimchukie mwenzako kutokana na hali yake hiyo. Inawezekana kuwa kweli kazi zake ofisini zinamponza na kuathiri uwezo wake chumbani. Lakini siku ambazo hafanyi kazi anafaa kupumzika vya kutosha kwa lengo la kukutimizia mahitaji yako.
Sitaki kumrudia
Mambo shangazi? Nilikuwa nimeolewa lakini siku moja tukakosana na mume wangu na tukaachana. Sasa amekuwa akinipigia simu akitaka turudiane na mimi sitaki. Nishauri.
Kupitia SMS
Sijui unataka nikushauri namna gani kama tayari umeamua hutaki kurudi katika ndoa yako. Iwapo unahisi hamuwezi kuishi tena kwa amani na mwanamume huyo, basi msahau na uendelee na maisha yako.
Dadake ameolewa na mjomba wangu
Shikamoo shangazi. Kuna mwanamke fulani kijijini ambaye amenasa hisia zangu kimapenzi na nilimdokezea hilo majuzi. Lakini aliniambia huenda haitawezekana kwa kuwa dada yake ameolewa na mjomba wangu. Nifanyeje?
Kupitia SMS
Uhusiano wa dada yake na mjomba wako hauwezi kuwa na athari zozote mbaya kwa uhusiano wenu. Hata hivyo, jamii tofauti zina desturi tofauti na huenda uhusiano wenu utakuwa kinyume na desturi za jamii yenu. Ni muhimu kuwauliza wanaojua kwanza ili mjue iwapo ni sawa au la.
Mwanafunzi wa shule yetu ameahidi tutafunga ndoa
Shangazi hujambo? Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na nimependana na mwanafunzi mwenzangu. Ameniahidi kuwa tutaoana tukimaliza masomo. Je, Inawezekana?
Kupitia SMS
Mwenzako amekuahidi tu na ana haki ya kubadili nia yake baadaye kwa sababu huna mamlaka juu yake. Pili, nyinyi bado ni vijana na hamjui hasa maana ya mapenzi na ndoa. Sina uwezo wa kutabiri iwapo itawezekana au haitawezekana. Itabidi usubiri tu, utajua ukweli wakati huo ukifika.
Mume hunitandika
Shangazi pokea salamu zangu. Nimekuwa katika ndoa kwa miaka sita. Lakini nimelazimika kutorokea kwa wazazi wangu pamoja na watoto wangu kutokana na mume wangu kunidhulumu kwa kunipiga. Nimeapa sitarudi hadi aje tuketi chini na wazazi tusuluhishe jambo hilo. Nishauri.
Kupitia SMS
Hatua na msimamo ambao umechukua ni sawa kabisa. Hakuna aliye na haki ya kumdhulumu mwenzake katika ndoa na hali inapokifikia hiyo huwa ni heri kuachana. Asipojirekebisha muondokee ujiepushe na dhuluma na aibu.
Amehepa baada ya kumwonjesha asali
Vipi shangazi? Juzi nilimshawishi mpenzi wangu tukarusha roho kwa mara ya kwanza tangu tulipojuana miezi kadhaa iliyopita. Tangu wakati huo sijamuona wala kumsikia, nimekuwa nikimpigia simu bila jibu. Kuna nini?
Kupitia SMS
Inawezekana kwamba mwenzako hakufurahia ulivyompeleka katika shughuli hiyo na sasa hataki lolote kukuhusu wewe. Hata hivyo, ikiwezekana mtafute akuelezee.