Njaa mahindi yakioza
WAKULIMA Kaskazini mwa Rift Valley, wanahesabu hasara baada ya mahindi yao kuanza kuoza kwa kukosa mahala pa kuyauza, huku Shirika la Msalaba Mwekundu (KRCS) likikubali kuwa watu kadhaa wamekufa kutokana na njaa.
“Watu wamekufa kutokana na sababu tofauti ikiwa ni pamoja na njaa na ukame,” alisema Katibu Mkuu wa KRCS, Abbas Gullet mnamo Alhamisi.
Tangazo hilo linalingana na lile la Gavana John Lonyangapuo wa Pokot Magharibi, ambaye amesema kuwa watu wawili wamekufa kwa njaa katika kaunti yake. Machifu, madiwani na wanahabari pia wamesisitiza kuwa watu wanakufa kwa sababu ya njaa katika kaunti za Turkana na Baringo.
Lakini maafisa wa Serikali wakiongozwa na Naibu Rais William Ruto wamesisitiza hakuna Mkenya yeyote aliyepoteza maisha kwa kukosa chakula. Maoni hayo yameungwa mkono na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa.
Vigogo hao wa serikali wamewalaumu wanasiasa mashinani, machifu na wanahabari kwa madai ya kueneza uvumi na kuzua taharuki.
“Kumekuwa na taarifa nyingi za uongo kuhusiana na yale yamekuwa yakitokea. Tumeambiwa kuwa watu 11 wamefariki lakini hilo sio kweli. Hakuna mtu yeyote ambaye amefariki kwa sababu ya njaa,” akasema Dkt Ruto mnamo Jumatano.
“Hakuna kifo chochote ambacho kimethibitishwa kusababishwa na njaa,” akasema Bw Wamalwa mnamo Jumanne.
Walisema hayo huku Gavana John Lonyangapuo wa Pokot Magharibi akithibitisha kuwa watu wawili wamefariki katika eneo lake.
Akiongea Alhamisi, Bw Gullet alisema watu 1.1 milioni wanakabiliwa na njaa, na idadi hiyo inazidi kuongezeka, na shirika kuwa lake linalenga kukusanya Sh824.6 milioni kusambaza misaada.
Kinaya
Kinaya ni kwamba wakulima wa mahindi eneo la North Rift wanasema serikali imeacha kununua mahindi na sasa yameanza kuharibika.
“Nilivuna magumia 3,000 lakini nilifaulu kuuza 1,000 kwa Bodi ya Taifa ya Nafaka na Mazao (NCPB). Sikuweza kuuza mengine kwa sababu ya masharti makali,” alisema mkulima Jackson Too kutoka Moiben, Kaunti ya Uasin Gishu.
Kwa sasa bei ya mahindi imeshuka hadi Sh1,500 kwa gunia la kilo 90, huku wakulima wakilazimika kuyauza kwa bei hiyo ili wapate pesa za kununua pembejeo kabla ya msimu wa upanzi.
NCPB inanunua gunia ya kilo 90 kwa Sh2,500 lakini wakulima wengi wamefungiwa nje kufuatia masharti makali.
Bei hiyo imeshuka huku ile ya mbolea ikipanda hadi Sh3,500 baada ya Serikali kushindwa kuagiza fatalaiza ya bei nafuu ambayo ingeuzwa Sh1,500 kwa gunia la kilo 50.
Mahindi haya yanaoza katika kaunti za Uasin Gishu na Trans Nzoia, ambazo zimo karibu na Baringo na Turkana, ambako takriban watu 11 wamekufa kutokana na njaa.