Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mzee anataka kunioa lakini naogopa kusemwa

March 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 23 na niliachana na mume wangu miaka mitatu iliyopita. Nimependana na mwanamume ambaye amenizidi umri kwa miaka 20 na yuko tayari kunioa. Nataka sana lakini naogopa kusemwa. Nishauri.

Kupitia SMS

Wewe sasa ni mtu mzima na una haki ya kujiamulia mambo yote kuhusu maisha yako. Ukikosa kufanya maamuzi kulingana na moyo wako kwa kuogopa kusemwa utakosa mengi mazuri. Isitoshe, hata ufanye nini, binadamu watakusema tu. Fuata moyo wako na uishi maisha yako.

 

Hataki kusubiri nimalize masomo

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 17 na ninasoma katika shule ya upili. Kuna kijana jirani yetu mtaani ambaye ananipenda nami pia nampenda. Hata hivyo, sitaki kujifunga katika uhusiano huo kwa sasa kwa sababu sitaki uniharibie masomo yangu. Nimemwambia asubiri nikamilishe safari yangu ya masomo lakini amekataa. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni muhimu unaelewa kuwa ukijiingiza katika uhusiano wa mapenzi unaweza kuathiri vibaya masomo yako. Kama huyo anayedai kukupenda hataki kusubiri, huna haja ya kumbembeleza. Mwambie angojee iwapo kweli anakupenda la sivyo atafute mwingine. Utakapokuwa tayari utampata mwingine.

 

Tuliachana lakini bado nampenda

Kwako shangazi. Niliolewa kwa miaka miwili lakini tukaachana na mume wangu. Nimekutana na wanaume kadhaa ambao wananitaka lakini hakuna kati yao ninayempenda kama aliyekuwa mume wangu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Hakuna mtu anayefanana na mwenzake wala huwezi kumpata aliye kama mume wako mliyeachana. Kama hakuna uwezekano wa kurudiana naye, itabidi ubadili msimamo wako na kuolewa na mwingine la sivyo ina maana utaishi bila mume.

 

Nimemzidi umri

Kwako shangazi. Nilikuwa na mpenzi na akaniacha baada ya kuzaa watoto wawili pamoja. Umri umenisonga na nilikuwa nimekata tamaa ya kuolewa. Lakini nimebahatika kupata mchumba ingawa nimemzidi umri kwa miaka kadhaa. Yuko tayari kunioa ila nahofia kukataliwa na jamaa zake. Nishauri.

Kupitia SMS

Mwanamume mnayependana ni mtu mzima na ana haki ya kufanya uamuzi wowote kuhusu maisha yake. Kama amekupenda nawe unampenda, sijui ni kwa nini unajali kuhusu jamaa zake kwani mke ni wa mumewe wala si wa jamii. Msaidie katika kutimiza ndoto yake ya kuwa mume wako na baba ya watoto wako.

 

Ninaumia moyoni kwa kuachwa ghafla

Shangazi ninahitaji ushauri wako. Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke fulani kwa miaka miwili. Ninampenda sana na amekuwa sehemu muhimu katika maisha yangu ya kila siku. Sasa ameniacha ghafla bila sababu. Uamuzi wake huo umeniumiza sana moyoni, sijuia maisha yangu yatakuwaje bila kuwa naye.

Kupitia SMS

Bila shaka mpenzi wako alikuwa na sababu zake mwenyewe za kufikia uamuzi wake huo. Inawezekana amepata mwingine ama ameamua tu kuwa hataki tena kuendelea na uhusiano huo. Ni heri umtafute uzungumze naye ili ujue sababu hasa ya uamuzi wake huo wa ghafla, na uwe tayari kuendelea na maisha yako.

 

Nitamtoa wapi mwanamume mwaminifu?

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 20 na nimetafuta mpenzi kwa muda mrefu. Tatizo ni kuwa nimekosa mwanamume ninayeweza kuamini kwa sababu nimeshikana na kadhaa na kugundua baadaye kuwa wana uhusiano na wanawake wengine. Naelekea kukata tamaa, tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Nyakati tunazoishi zina walaghai wengi wa kimapenzi, si wanaume tu bali pia wanawake. Naona wewe bado ni msichana mdogo kiumri niseme hivyo; kwa hivyo una muda wa kutosha wa kutafuta anayekufaa. Kuwa na subira na makini na hatimaye utapata.