26/06/2019

Wakataa kutoa mahari hadi binti aolewe na kuzaa

SABATIA, VIHIGA

Kizaazaa kilizuka eneo hili baada ya mashemeji watarajiwa kuwatawanya wazee waliokuwa wakijadili harusi ya kijana wao kwa kudinda kutoa mahari hadi binti aolewe na kuzaa.

Inadaiwa kwamba makalameni waliamua kuwatawanya wazee hao wakiwalaumu kwa kutumia maneno yaliyowakosea heshima pamoja na dada yao kwa kudai lazima awathibitishie ana uwezo wa kuzaa.

Inasemekana bw harusi alikuwa ameitisha kikao na wazee wa familia nyumbani kwake ili kujadili mambo muhimu. Kikaoni, walikuwa mashemeji watarajiwa wa bi harusi ambao walikuwa wamealikwa.

Kulingana na mdokezi, wazee walipokuwa wakitoa hoja zao, mzee mmoja alisimama na kupinga kutolewa kwa mahari yote hadi mrembo atakapoolewa na hata kuwazalia watoto wawili.

“Hatuwezi kutoa mahari yote kwa sasa. Msichana lazima aolewe mwanzo na pia tuhakikishe kuwa ana uwezo wa kutupa wajukuu ndiposa tukamilishe mahari,” mzee mmoja alisema.

Duru zinasema makalameni waliinuka kwa pamoja na kumuonya mzee yule. “Una ushamba sana wewe. Hauwezi kusema hivyo tukiwa hapa. Tuheshimu pamoja na dada yetu,” kalameni mmoja aliteta.

Inadaiwa kwamba mzee mwingine alisimama na kumuunga mkono mzee mwenzake.

“Sisi wazee tunazungumza kwa busara. Kile ambacho kimesemwa hapa ni ukweli usiopingika kabisa,” alieleza.

Habari zilizotufikia zinasema makalameni walielekea walikokuwa wameketi wazee wale na kuwaamrisha waondoke mara moja.

“Kile mmesema hapa hakina busara wala mashiko yoyote. Vichwa vyenu vimejaa upepo. Ondokeni hapa,” makalameni waliwafokea wazee.

Duru zinasema wazee walisita kutii amri. “Hamkutuita hapa kuja kusikia haya. Leo mtatujua,” mapolo walionya.

Inadaiwa wazee walipoona mapolo wakichomoa viboko, wote walilazimika kukimbilia usalama wao.