• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
JAMVI: Dhana Raila atawania urais 2022 yazua hofu   ya mgawanyiko Nasa

JAMVI: Dhana Raila atawania urais 2022 yazua hofu ya mgawanyiko Nasa

Na BENSON MATHEKA

Kwa ufupi:

  • Dalili zinaonyesha kuwa Bw Odinga amekuwa akitengwa na wenzake tangu ajiapishe kuwa rais wa wananchi
  • Wabunge wa ODM wanatumia kiapo kuwadhalilisha vinara wenza wa NASA ili kupata sababu ya kujiondoa NASA  na kuunda muungano mpya
  • Kulingana na Bw Ayub Savula, Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula wameanza kuweka mikakati mipya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022
  • Wabunge wa ODM wanahisi kwamba Kalonzo, Mudavadi na Wetangula waliwavunja moyo kwa kususia kuapishwa kwa Bw Odinga
  • Dalili kwamba hali sio shwari katika NASA zimejitokeza katika bunge vyama hivyo vilipopigania nafasi za uwakilishi katika kamati mbalimbali

Hofu kwamba huenda kinara wa NASA Raila Odinga akaamua kugombea urais tena 2022 kinyume na mkataba baina yake na vinara wenza, inayumbisha meli ya muungano huo na kuipa Jubilee mteremko kwa kukosa upinzani thabiti wa kukosoa utawala wa Rais Kenyatta.

Japo vinara wa muungano huo akiwemo Bw Raila, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula wamekuwa wakisisitiza kuwa wangali wameungana, wadadisi wanasema matukio ya hivi majuzi yanaonyesha kuwa kuna hofu na kutoaminiana katika NASA.

Kulingana na Bw Geff Kamwanah, mdadisi wa siasa ambaye amekuwa akifuatilia shughuli za NASA, dalili zinaonyesha kuwa Bw Odinga amekuwa akitengwa na wenzake tangu ajiapishe kuwa rais wa wananchi katika bustani ya Uhuru Park mnamo Januari 30.

“Kauli za vinara wenzake tangu wakose kuhudhuria hafla hiyo na washirika wao wa kisiasa zinaonyesha kwamba kuna shida katika NASA. Shida inatokana na hofu kwamba huenda Bw Odinga akawaruka na kugombea urais kwenye uchaguzi wa 2022 kinyume na walivyokubaliana,” asema Bw Kamwanah. Anasema ni wazi kuwa Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula hawakuunga kiapo cha Bw Odinga.

“Ni wazi kuwa wanasiasa wa ODM ya Bw Odinga ndio waliokuwa wakishinikiza kiapo hicho. Wakati mmoja mwenyekiti wa Wiper Kivutha Kibwana na katibu wa Amani National Congress Barack Muluka walilalamika kuwa ODM haikuwa ikiwahusisha katika maandalizi ya hafla hiyo na katika masuala mengine ya muungano wa NASA,” asema.

Kulingana na wadadisi, wabunge wa ODM bado wanairejelea hafla hiyo katika juhudi za kuwadhalilisha vinara wenza wa NASA ili kupata sababu ya kujiondoa NASA  na kuunda muungano mpya ambao Bw Odinga atatumia kugombea urais 2022.

“Mito ya kumtaka Bw Odinga kuwatema vinara wenzake kwa kususia kiapo chake ni njama pana ya kuvunja NASA na kukwepa mkataba wa NASA ambao aliahidi kutogombea urais tena,” aeleza Bw Kamwanah.

 

Vyama vinatoshana

Akihojiwa na runinga ya NTV mapema wiki hii, Bw Mudavadi alisema NASA si mali ya chama kimoja  bali inashirikisha vyama vinne na hakuna kikuu kuliko kingine.

Kiongozi huyo wa chama cha ANC alisema kilicho muhimu ni kupanga mikakati ya uchaguzi wa 2022.

Ishara kwamba kuna hofu ya Bw Odinga kugombea urais tena ilionekana hata kabla ya kuapishwa kwake kwenye mkutano wa bunge la wananchi mjini Machakos Bw Kibwana alipomtaka kuheshimu mkataba wa NASA na kumuunga mkono Bw Musyoka kwenye uchaguzi wa 2022.

Akimjibu, Bw Odinga alisema lililo muhimu ni kukomboa ushindi ambao NASA inaamini ilipokonywa na Jubilee kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 8, 2017.

“Jibu la Bw Odinga katika ngome ya Wiper halikuwafurahisha wanachama na viongozi wa chama hicho. Ukweli wa mambo ni kuwa chama chetu kilichukulia kauli yake kama thibitisho kwamba hatamuunga kiongozi wetu ambaye amekuwa akimuunga tangu 2013,” anasema mbunge mmoja wa Wiper ambaye aliomba tusichapishe jina lake kwa sababu si msemaji wa chama hicho.

Kulingana na mbunge wa Lugari, Bw Ayub Savula, Bw Musyoka, Bw Mudavadi na Bw Wetangula wameanza kuweka mikakati mipya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

 

Mchujo

“Ajenda yetu ya kwanza ni haki katika uchaguzi, ya pili ni kuwa na mchujo kati ya Bw Musalia na Bw Kalonzo katika uchaguzi wa 2022,” Bw Savula alinukuliwa akisema. Hata hivyo alisema ANC imejitolea kuimarisha NASA.

Wadadisi wanasema wabunge wa ODM wanahisi kwamba Kalonzo, Mudavadi na Wetangula waliwavunja moyo kwa kususia kuapishwa kwa Bw Odinga.

Bw Kamwanah anasema japo kuna hofu na kutoaminiana katika NASA, vyama tanzu vinakubaliana kwamba adui vinayemlenga ni Jubilee.

“Wanasema kwamba adui wa NASA ni  Jubilee na watafanya kila wawezalo ili vinara wote waendelee kuungana. Hata hivyo, huenda adui ni NASA yenyewe,” alisema.
Kulingana na mbunge mwingine wa chama hicho ambaye aliomba tusitaje jina lake, kuna hisia kwamba huenda Bw Odinga akatema NASA kuunda muungano mpya.

“Umewasikia wabunge wa chama chake wakimtaka awaache wenzake kwa kukataa kuhudhuria kuapishwa kwake, hii ni njama ya kukwepa makubaliano yake na vinara wenzake. Akifanya hivyo, utakuwa mwisho wa NASA,” asema mbunge huyo.

 

Usaliti

Mbunge wa Nyando, Bw Jared Okello mmoja wa wanaomtaka Bw Odinga kuunda muungano mpya wa kisiasa anasema wenzake katika NASA walimsaliti kwa kususia kuapishwa kwake.

“Ninasisitiza kuwa Raila Odinga anafaa kutafuta washirika wengine wa kisiasa. Kumuacha rais wa wananchi wakati muhimu wa kutawazwa kwake kulikuwa kitendo cha usaliti na woga.

Vinara hao wengine walikuwa humu nchini  na hakuna aliyekuwa mgonjwa mbali na kufahamu kuwa angeapishwa,” Bw Okello aliambia wanahabari siku tano baada ya  Bw Odinga kuapishwa.

Bw Kamwanah anasema kwamba dalili kwamba hali sio shwari katika NASA zimejitokeza katika bunge vyama hivyo vinapopigania nafasi za uwakilishi katika kamati mbalimbali.

“Hii ni fursa ambayo Jubilee itatumia kufanikisha sera zake kwa sababu upinzani hautakuwa na nguvu za kukosoa serikali,” asema.

You can share this post!

BI TAIFA FEBRUARI 23, 2018

JAMVI: Dhamira fiche ya Uhuru kuzuia wabunge wa Jubilee...

adminleo