• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
ULIMBWENDE: Njia ya kiasili ya kuondoa michirizi

ULIMBWENDE: Njia ya kiasili ya kuondoa michirizi

Na MARGARET MAINA

[email protected]

MICHIRIZI ‘stretch marks’ hutokea sehemu mbalimbali mwilini kama mikononi, miguuni, mapajani au tumboni.

Alama hizi hutokea baada ya sehemu ya kati ya ngozi, kutanuka ghafla ndani ya muda mfupi pengine kwa sababu ya mazoezi makali au mtu kuongezeka uzani ghafla.

Pia kuna baadhi ya dawa au homoni ambazo kwa namna moja au nyingine huathiri tishu za ngozi na hivyo kumfanya mtu akapata alama za michirizi.

Ujauzito kwa baadhi ya wanawake na pia hali itokanayo na kurithi kutoka kwa watu wa familia pia inachangia mtu kupata alama hizi katika ngozi yake.

Kwa ufupi, michirizi inasababishwa na:

– Ujauzito

– Kuongezeka kwa mwili (unene)

– Ukuaji wa haraka wakati wa kubalehe

– Mabadiliko ya mwili

– Lishe mbovu

 

Kwa kawaida, michirizi haimletei mtu maumivu yoyote, bali jambo kubwa huwa ni kuubadili muonekano wa ngozi ya mtu.

Kwa baadhi ya watu michirizi huwa ni mikubwa sana, na kwa namna moja au nyingine humnyima mtu uhuru au humfanya mtu asiwe na amani anapokuwa mbele ya watu kwa kutegemea michirizi hiyo imetokea sehemu gani ya mwili.

Unaweza kuondoa michirizi kwa njia za kiasili kwa kutumia:

Kahawa

Mbegu za kahawa zilizokaangwa kiasi robo kikombe. Saga kahawa hiyo. Ukishasaga na kupata ule unga, uchanganye kwenye losheni ya mikono yako na kisha uipake palipo na michirizi.

Haina madhara, ipake mara mbili hadi tatu kwa siku. Futa kwa kitambaa na maji ya fufutende. Mchanganyiko huu pia waweza ukautumia kama ‘facial’ ambayo inasaidia ngozi kutozeeka au mikunjo ya ngozi kupunguka au kumalizika kabisa.

Juisi ya limau na tango

Angalau unahitaji limau moja na tango kipande kidogo. Chuja juisi ya limau kisha changanya na kipande cha tango na uvisage pamoja. Paka mchanganyiko huu kwenye eneo ilipo michirizi na ukae nayo kwa muda wa dakika 10 kisha osha.

Hii ni nzuri pia kuondoa hata madoa usoni kwa wenye ngozi za mafuta. Unaweza itumia usoni pia. Fanya hivi kila siku.

 

Viazi mviringo

Unapaswa kuvikata vipande vidogovidogo vya viazi hivyo kisha uvitumie kusugua sehemu yenye michirizi. Tulia kwa muda kisha oga kwa kutumia maji ya ufufutende. Fanya hivi angalau kila siku.

 

Ni muhimu uzingatia kula lishe bora na kunywa maji mengi; angalau glasi nane kwa siku.

Ulaji wa mboga za majani na vyakula vyenye wingi wa vitamini C na E na madini ya Zinc na Silica ikiwamo karoti,spinachi na maharage mabichi pia ni muhimu.

You can share this post!

Emerging Stars kikaangoni kufukuzia tiketi ya Olimpiki

Ujerumani yalaza Uholanzi mechi ya kufuzu Euro

adminleo