Wanariadha 582 kunogesha mbio za Nyika za Dunia
HUKU mabingwa watetezi Kenya wakizamia mazoezi yao ya mwisho kabla ya kuelekea nchini Denmark kwa Mbio za Nyika za Dunia, Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) limetoa orodha ya mataifa shiriki na wawakilishi wao pamoja na tuzo ya makala hayo ya 43.
Katika taarifa yake, IAAF imesema kwamba wakimbiaji 582 kutoka mataifa 67 watashuka mjini Aarhus kuwania ubingwa hapo Machi 30.
Wanariadha 557 kutoka mataifa 60 walishiriki makala ya mwaka 2017 jijini Kampala nchini Uganda ambako Kenya ilirejesha taji ambalo mahasimu wao wa tangu jadi Ethiopia walikuwa wamewapokonya mwaka 2015.
Zaidi ya wakimbiaji 300 wamejiandikisha kutimka katika vitengo vya watu wazima ambavyo mwaka 2017 Kenya ilinyakua mataji kupitia kwa Geoffrey Kamworor na Irene Cheptai.
Kamworor alifuzu kutetea taji la mbio za nyika za wanaume za kilomita 10 ambazo atakuwa akivizia kuwa mfalme kwa makala ya tatu mfululizo.
Kenya imekuwa ikifanyia matayarisho yake katika Chuo cha Ualimu cha Kigari katika kaunti ya Embu kwa wiki tatu sasa. Imeshinda mataji ya binafsi ya vitengo vya watu wazima vya wanaume na kinadada tangu mwaka 2015.
Wakimbiaji 200 walio chini ya umri wa miaka 20 pia watakuwa mjini Aarhus kutafuta ufanisi katika mbio za kilomita nane (wanaume) na kilomita sita (wanawake).
Vilevile, kuna kitengo cha kupokezana vijiti ambacho timu zinahitajika kuwa na kikosi kinachojumuisha wanaume kwa wanawake.
Shirikisho la IAAF limetangaza kwamba washindi wa mataji ya binafsi katika mbio za watu wazima watatunikiwa Sh3 milioni kila mmoja.
Nambari mbili hadi sita watatia mfukoni Sh1.5 milioni, Sh1 milioni, Sh705000, Sh504000 na Sh302000, mtawalia.
Wanne tu
Wakimbiaji wanne wa kwanza kukamilisha mbio kutoka taifa moja ndio watakaopata alama.
Zawadi ya kuwa timu ya kwanza ni Sh2 milioni. Nambari mbili hadi sita watatuzwa Sh1.6 milioni, Sh1.2 milioni, Sh1 milioni, Sh806000 na Sh403000, mtawalia.
Nafasi nne za kwanza katika mbio za nyika za mseto zitaandamana na tuzo ya Sh1.2 milioni, Sh806000, Sh605000 na Sh403000, mtawalia.
Vitengo vya wakimbiaji walio chini ya umri wa miaka 20 havina tuzo za kifedha, bali medali pekee.
Kikosi cha Kenya: Wanaume kilomita 10 – Geoffrey Kamworor, Rhonex Kipruto, Evans Kiptum, Amos Kirui, Rodgers Kwemoi, Charles Simotwo, Paul Tanui na Richard Yator; Wanawake kilomita nane – Beatrice Chepkoech, Eva Cherono, Margaret Chelimo, Beatrice Mutai, Hellen Obiri, Lilian Kasait, Deborah Samum na Agnes Jebet; Wanaume kilomita nane – Leonard Bett, Edwin Bett, Emmanuel Korir, Charles Lokir, Samuel Masai na Cleophas Kandie; Wanawake kilomita sita – Beatrice Chebet, Mercy Jerop, Mercy Kerarei, Betty Kibet, Lydia Jeruto na Jackline Rotich.