KAULI YA WALIBORA: Kongamano kuhusu ugaidi Iraki lilivyonitoa uziwi kuhusu Kiarabu
Na KEN WALIBORA
KIARABU hiki kina nini?
Mtu mmoja, mkereketwa mkubwa wa Kiswahili aliwahi kunisuta sana kwa kuwa sikijui Kiarabu.
Alitoa cheche kalikali,kama watoavyo cheche wakereketwa waliokeretwa na kukeketwa maini, akidai kwamba kwa vile sikijui Kiarabu basi siwezi kukijua Kiswahili.
Ukichunguza kwa makini utauhukumu msimamo wake kuwa sugu, msimamo usiopindika wala kubadilika.
Na maskini nimejikuta Arabuni tangu majuzi yale, nimefunikwa gubigubi na uzumbukuku wangu, umenifunika si haba, sijui be wala te ya Kiarabu.
Nimekuja kuhudhuria na kuhutubia kongomano kuhusu ugaidi lenye kaulimbiu “Ulimwengu bila Ugaidi,” (ingawa mimi si gaidi wala bingwa kuhusu masuala ya ugaidi).
Nilimwambia rafiki yangu mmoja kwa njia ya WhatsApp kwamba nipo Baghdad, Iraki.
Akashtuka sana: “Upo nje ya Saddam Hussein na Abunuwasi!”
Naam, makala hii safari hii naiandikia kwenye kingo za mto Taigrisi unaotajwa katika Biblia katika kitabu cha Mwanzo katika yale masimulizi ya Shamba la Edeni.
Kabla ya kuondoka Nairobi nilipowauliza wanafunzi wangu wa Taaluma za Mahusiano ya Kimataifa, Chuo Kikuu cha Riara niwaletee nini kutoka Iraki, waliniambia “Jilete Wewe mwenyewe. Tunakuombea urejee salama u salimini, hiyo ndiyo zawadi pekee itakayokidhi utashi wetu.”
Basi mimi huyu na Kiarubu karibu na sifuri. Maneno ya Kiarabu yamenizunguka. Mara moja moja nasikia na kudhani wanasema Kiswahili hasa nimepowasikia wakisema maneno kama vile “shukran, nusu, jamhuriya, Rais, na samak.” Lakini hili kutokujua Kiarabu si kubwa, kubwa ni kusoma nikiwa hotelini Baghdad lile onyo linalotolewa na Marekani kwa raia zake, “Msisafiri Iraki.” Ilani hiyo inaendelea kusema:
- Andika wasia na kufafanua ni nani atafaidi kutokana na bima yako ya maisha au nani atakuwa mfawidhi wa bima hiyo.
- Jadili na familia yako kuhusu utunzaji wa watoto, wanyama vipenzi, mali na vitu vinginevyo unavyovimiliki, matamanio ya mazishi yako, na kadhalika.
- Waonyeshe wengine stakabadhi, nywila zako au nambari za siri na mambo mengine muhimu yakayowawezesha wapendwa wako kuyasimamia mambo yako ikiwa utashindwa kurejea Marekani kama ulivyopanga.
Baada ya kusoma habari hizi nilitaka kubadili neno Marekani kuwa Kenya.
Nikawauliza wahudumu wa hoteli kama ninaweza kutoka hotelini niende zangu nikatembee katika barabara za Baghdad niwaone Wairaki halisia.
“Ukiondoka nje huwezi kurudi tena,” wanasema bila tabasamu. Natafuta fimbo baada ya kuumwa na nyoka nini?
***
Nilipokuwa mshereheshaji kwenye mahafali ya Chuo Kikuu cha Riara yaliyorushwa mbashara na NTV, nilitumia neno “Amidi wa Wanafunzi” kwa maana ya Dean of Students.
Nilitegemea maana pana ya “Amidi” kwa Kiswahili kulingana na utaratibu uliotolewa na Taaasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Na ieleweke kwamba Dean anayesimamia kitivo na tunamwita “Mtiva.” Dean wa shule kuu (school katika chuo kikuu) ndiye “Amidi.” Ingawa sikukosea kumtaja Dean of Students kama “amidi wa wanafunzi,” tafsiri waliyoipendekeza TATAKI kwa Dean of Students ni “mshauri wa wanafunzi.”