• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
AK yadumisha Pogisho na Kiprop kwa mbio za Afrika

AK yadumisha Pogisho na Kiprop kwa mbio za Afrika

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) limewarejesha timuni watimkaji Reuben Pogisho na Jacob Kiprop ambao awali walikuwa wametemwa licha ya kuibuka washindi wa mbio za mita 5,000.

Wawili hao kwa sasa watakuwa sehemu ya kikosi kitakachopeperusha bendera ya Kenya kwenye Riadha za Masharikisho barani Afrika (CAA) kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20. Mbio hizo zitaandaliwa jijini Abidjan, Ivory Coast kati ya Aprili 13-20, 2019.

Mwenyekiti wa Kamati ya AK Youth Barnaba Korir amekiri kwamba tukio lililowashuhudia wanariadha Francis Lagat na Victor Chepkwony wakishindana peke yao baada ya kukosa nafasi ya kuunga kikosi cha mwisho ni la kusikitisha.

Lagat na Chepkwony ambao walikosekana katika orodha ya mwisho walikubaliwa kushindana wao kwa wao baada ya rufaa yao kuidhinishwa. Mwishowe, wawili hao walisajili muda bora na wa kasi zaidi wa dakika 14:10.5 na 14:16.7 mtawalia.

Ni matokeo ambayo yalitosha kuwadengua Pogisho na Kiprop ambao awali walikuwa wameandikisha muda wa dakika 14:23.6 na 14:25.0 mtawalia. Kuondolewa kwa wawili hao orodhani kulizua hisia kali miongoni mwa mashabiki na wakufunzi wa wanariadha hao.

Kwa mujibu wa Korir, uchunguzi wa kina kuhusu ripoti za fainali za mchujo huo ulibainisha kwamba baadhi ya makocha na maafisa walishiriki udanganyifu katika kuyafikia mengi ya maamuzi yao.

Korir alifchua kwamba ripoti hiyo tayari imewasilishwa kwa Rais wa AK Jackson Tuwei na Mkurugenzi wa Mashindano Paul Mutwii kwa utathmini wa ziada.

Mapambano ya CAA U-20 yataandaliwa sawia na riadha za chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18 jijini Abidjan.

AK iliandaa michujo ya kuteua vikosi vitakavyowakilisha Kenya katika mashindano hayo mawili uwanjani MISC Kasarani mnamo Alhamisi na Ijumaa wiki jana.

Hata hivyo, Korir alitetea kujumuishwa kwa Leonard Bett na Lydia Jeruto kwenye kikosi cha Kenya. Bett ni mshikilizi wa nishani ya fedha katika mbio za dunia za mita 3,000 kuruka maji na viunzi kwa chipukizi wa U-20. Kwa upande wake, Jeruto aliibuka mshindi wa medali ya fedha katika mbio za dunia za mita 800 kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 18.

Wawili hao ambao kwa sasa wamo kambini mwa kikosi cha Kenya hawakushiriki mchujo wa kitaifa wa Mbio za Nyika mjini Eldoret mwishoni mwa Februari.

Wataungana na kikosi cha Kenya jijini Abidjan mwishoni mwa Mbio za Nyika za Dunia zitakazoandaliwa jijini Aarhus, Denmark mnamo Machi 30.

Kenya imekuwa ikifanyia matayarisho yake katika Chuo cha Walimu cha Kigari, Embu kwa minajili ya Makala ya 43 ya mbio hizo mwaka 2019.

Imeshinda mataji ya binafsi ya vitengo vya watu wazima vya wanaume na kinadada tangu 2015.

Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) limetangaza kwamba washindi wa mataji ya binafsi katika mbio za watu wazima watatunikiwa Sh3 milioni kila mmoja. Nambari mbili hadi sita watatia mfukoni Sh1.5 milioni, Sh1 milioni, Sh705,000, Sh504,000 na Sh302,000 mtawalia.

Wanne

Wakimbiaji wanne wa kwanza kukamilisha mbio kutoka taifa moja ndio watakaopata alama. Zawadi ya kuwa timu ya kwanza ni Sh2 milioni. Nambari mbili hadi sita watatuzwa Sh1.6 milioni, Sh1.2 milioni, Sh1 milioni, Sh806000 na Sh403000, mtawalia.

Nafasi nne za kwanza katika mbio za nyika za mseto zitaandamana na tuzo ya Sh1.2 milioni, Sh806000, Sh605000 na Sh403000, mtawalia.

Vitengo vya wakimbiaji walio chini ya umri wa miaka 20 havina tuzo za kifedha, bali medali pekee.

Kikosi cha Kenya:

Wanaume kilomita 10 – Geoffrey Kamworor, Rhonex Kipruto, Evans Kiptum, Amos Kirui, Rodgers Kwemoi, Charles Simotwo, Paul Tanui na Richard Yator; Wanawake kilomita nane – Beatrice Chepkoech, Eva Cherono, Margaret Chelimo, Beatrice Mutai, Hellen Obiri, Lilian Kasait, Deborah Samum na Agnes Jebet; Wanaume kilomita nane – Leonard Bett, Edwin Bett, Emmanuel Korir, Charles Lokir, Samuel Masai na Cleophas Kandie; Wanawake kilomita sita – Beatrice Chebet, Mercy Jerop, Mercy Kerarei, Betty Kibet, Lydia Jeruto na Jackline Rotich.

You can share this post!

SHANGAZI AKUJIBU: Amesaliti penzi na hata kapata ujauzito,...

Gor waendea Zoo, Tusker ikiwaalika Sharks gozini KPL

adminleo