Habari

Mrengo wa Ruto wakaza kamba

March 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA na BENSON MATHEKA

LICHA ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kukutana na kuonekana kupoesha joto la kisiasa ndani ya chama cha Jubilee, washirika wa Bw Ruto wanaendelea kukosoa wenzao wanaounga muafaka na vita dhidi ya ufisadi.

Wandani wa Dkt Ruto wanadai wenzao wameacha kuvumisha maslahi ya Jubilee na badala yake wanashirikiana na wabunge wa ODM kuhujumu umoja katika chama hicho.

Walisema ajenda kuu ya Wabunge hao ni kuendeleza maslahi ya kisiasa ya kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kizingizio kwamba wanamtetea Rais Uhuru Kenyatta.

“Tulifurahi mkutano kati ya Rais Uhuru Kenyatta na Dkt Ruto kwani walidhihirisha kwamba wanafanya kazi pamoja kuendeleza ajenda za Jubilee ilivyoratibiwa katika manifesto yake. Lakini tunawaonya kukoma kushirikiana na wale wa upinzani kuhujumu ndoto ya Dkt Ruto ya kuingia Ikulu 2022 kwa kuleta hoja ya kumuondoa mamlakani,” Mbunge wa Kandara Alice Wahome alisema Ijumaa.

“Hatuwaruhusu wabunge hawa, wakiongozwa na Maina Kamanda kushirikiana na marafiki wao wa chama cha ODM kuendeleza kampeni ya kumtusi Naibu Rais kila wikendi wakijifanya eti wanahudhuria ibada za kanisa,” akaongeza na kumtaja Bw Kamanda na wenzake kama “waasi”.

Bw Kamanda, ambaye ni mbunge maalumu wa Jubilee amekuwa akiendeleza kampeni za kumtaka Dkt Ruto ajiuzulu kwa kupinga vita dhidi ya ufisadi.

Mbunge wa Sirisia John Waluke pia alimtetea Dkt Ruto akisema anapakwa “tope la ufisadi bila sababu, akisema vita hivyo vimeingizwa siasa.

“Tunaunga mkono vita dhidi ya ufisadi lakini visitumiwe kulenga kuzima ndoto ya Ruto kuingia Ikulu” “Bado tunaamini Rais Kenyatta ana imani na uwezo na utendakazi wa naibu wake hadi akamtembelea afisini mwake wiki hii. Kwa hivyo, wale wanaotaka kuleta mgawanyiko ndani ya Jubilee kwa kutumia handsheki tunawaambia wakome kabisa,” aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano ya simu.

Rekodi

Naye Mbunge maalumu Bw David Sankok alielezea imani kuwa Dkt Ruto ataingia Ikulu 2022, akisema wale wote wanaompinga watafyekwa kwa “upepo wa rekodi yake ya maendeleo”.

“Mimi ndiye jabali wa Team Tanga Tanga katika eneo la Maa. Na hapa sote tuko nyuma ya Dkt Ruto. Wale wengine wakome kutuingilia,” akasema.

Ijumaa, Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu na mwenzake wa Nakuru Lee Kinyanjui waliungana na wabunge tisa kulaumu wanaotaka Ruto atimuliwe.

Wakiongea mbele ya Ruto mjini Nakuru, viongozi hao walisema mjadala huo unalenga kulemaza maendeleo ya Jubilee.

Mwishoni mwa wiki jana, Bw Kamanda pamoja na wabunge wengine tisa wa vyama vya ODM, Wiper na Jubilee walidai Dkt Ruto ndiye anayesababisha mivutano ndani ya Jubilee kwa kuingilia kazi ya Mkurugenzi wa DCI George Kinoti.