• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
UFISADI: Gavana Kasaine apigwa dhamana ya kihistoria

UFISADI: Gavana Kasaine apigwa dhamana ya kihistoria

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA ya Kuamua Kesi za Ufisadi Jumanne iliweka historia kwa kumwachilia Gavana wa Samburu Moses Kasaine Lenolkulal kwa dhamana ya juu zaidi ya Sh100 milioni pesa taslimu tangu Kenya ijinyakulie uhuru.

Dhamana hiyo iliyotangazwa na hakimu mkuu Douglas Ogoti iliwashtua watu wengi nchini.

Hata alipoachiliwa kwa dhamana hiyo, Gavana huyo alitabasamu tu kwa vile ni njia nyingine ya kunyimwa dhamana katika kesi inayomkabili ya upunjaji wa pesa za umma zipatao Sh84 milioni.

Endapo atashindwa kulipa dhamana hiyo ya pesa taslimu, Bw Ogoti alimwamuru Bw Lenolkulal awasilishe dhamana ya Sh150 milioni na madhamini mmoja wa kiasi sawa.

Gavana huyo alikanusha mashtaka manne ya kupokea pesa kwa njia ya ufisadi kwa kuruhusu kampuni yake Oryx Service Station kuuzia kaunti ya Samburu mafuta.

Bw Lenolkulal, ndiye Gavana wa pili kushtakiwa mahakamani baada ya Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong kwa ufisadi.

Kiongozi wa mashtaka Alexander Muteti akimosomea Gavana Lenolkulal mashtaka Aprili 2, 2019. Picha/ Richard Munguti

Gavana huyo ameshtakiwa pamoja na naibu wake Julius Lawrence Leseeto, Bw Stephen Siringa Letinina (katibu wa kaunti hiyo) na maafisa wakuu katika serikali yake.

Wengine wanaoshtakiwa pamoja na Gavana huyo ni Mabw Daniel Nakuo Lenolkirina, Josephine Naamo Lenasalia, Reuben Marumben Lemunyete , Linus Milton Lenolngenje, Paul Lolmuginani, Benard Ltarasi Lesurmat, Lilian Balanga, Andrew Ropilo Lanyasunya, David England Loosenge, Geoffrey Barun Kitewan na Hesbon Jack Ndathi.

Naibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Bw Alexander Muteti hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana ila aliomba masharti yawe makali.

Aliomba mahakama iamuru mshtakiwa azuiliwe kutekeleza majukumu yake kama Gavana kwa muda wa miezi 24 huku kesi ikiendelea.

Wakili Paul Nyamondi (kati) aliyemwakilisha gavana Lenolkulal. Picha/ Richard Munguti

Bw Muteti alisema sheria za kupambana na ufisadi zinawataka washukiwa wote wanaokabiliwa na mashtaka wasikubaliwe kuendelea kutekeleza majukumu yao hadi kesi isikizwe na kuamuliwa.

Bw Muteti alisema kuwa Bw Lenokulal “si tofauti na maafisa wengine wa serikali wanaozuiliwa kuendelea na kazi zao hadi kesi zinazowakabili zikamilike.”

“Kesi hii dhidi ya Bw Lenokulal ni ya kipekee kwa vile anashtakiwa kufanya biashara na kaunti anayoongoza,” alisema Bw Muteti.

Mahakama iliamuru washukiwa 13 ambao hawakufika kortini kujibu mashtaka wafike kortini Aprili 4, 2019.

Bw Ogoti aliamuru Gavana Lenokulal azuiliwe hadi atakapolipa dhamana hiyo.

 

You can share this post!

Akana kudukua akaunti za benki na kuiba Sh12 milioni

Kuniambia nitoe kafara ni upuuzi, Gavana Njuki aiambia...

adminleo