Lugha, Fasihi na ElimuMakala

KAULI YA WALIBORA: Kiswahili kitakua tu kwa ushirikiano, si ushindani mkali!

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na KEN WALIBORA

CHAMA cha Ukuzaji Kiswahili Duniani (CHAUKIDU) kiliasasisiwa mwaka wa 2012 nchini Marekani kwa lengo la kuchapusha usambazaji na ukuzaji wa Kiswahili kote duniani.

Uzinduzi wa chama ulifanyika katika mji wa baridi kali wa Madison, katika eneo la Maziwa Makuu Marekani.

Baadhi ya waasisi wa chama kama vile Kathrina Thompson (Zuhura), Charles Bwenge na Deo Ngoyani, hawakutaka hata kushika hatamu za uongozi wa chama tangu mwanzoni.

Walitaka kuanzisha chama kisha watu wengine wakiongoze hadi kifane kwa mafanikio makubwa.

Wale waliowania nafasi nao waliwania kwa nia ya kukiendeleza chama, si kujaza matumbo yao yasiyoshiba.

Baadhi yao hata hawakuwania nyadhifa, walipendekezwa tu na kupigiwa kura. Mimi nilikuwa miongoni mwa viongozi wa aina hiyo.

Nilijikuta tu kufumba na kufumbua nimekuwa Rais wa chama kipya. Ilikuwa muhimu kuweka msingi thabiti kwa chama na kwa ushirikiano na bodi na viongozi wengine hususan Katibu Mtendaji Mwalimu Leonard Muaka, tulijaribu kadri ya uwezo wetu.

Yalikuwa mambo ya msingi kama vile kusajili chama katika mfumo rasmi wa Marekani na kufungua akaunti ya benki, mambo tuliyoyatekeleza kwa hela zetu wenyewe.

Tulikuwa na mikutano kadha wa kadha ya kupanga mikakati ya mustakabali wa Kiswahili na chama cha CHAUKIDU. Tangu nimeondoka mamlakani wamefuatia marais wengine wawili, Prof Lioba Moshi na Prof Mahiri Mwita ambao mchango wao si haba.

CHAUKIDU kimepiga hatua kubwa. Baada ya makongomano ya awali yaliyofanyika Marekani, kimekuwa na makongomano Nairobi na Zanzibar na labda mwakani kutakuwa na kongomano Kampala, Uganda.

Mtoto aliyekuwa anakwenda dema, sasa anakimbia. Lakini zingatia kwamba nimesema mtoto; hajawa bado mtu mkubwa.

Ili kuhakikisha kwamba CHAUKIDU kinaendelea kupiga hatua zaidi, sharti watu wengine zaidi wajiunge nacho, wa nyumbani walio karibu na Maziwa Makuu ya Afrika Mashariki na vilevile wa ughaibuni hata wale walioko karibu na Maziwa Makuu ya Marekani au kwingineko.

Kipi kifanyike?

CHAUKIDU kinapaswa kushirikiana zaidi na wadau na vyama vinginevyo vya Kiswahili ili kukiendeleza Kiswahili. Ila napenda kuonya kwamba kwa sababu ya kuibuka kwa vyama vingi pembe zote duniani, hasa hasa Afrika Mashariki, ipo hatari ya kuzuka ushindani usiokuwa na sababu wala msingi.

Mara nyingine unahisi kana kwamba vyama vimeibuka kivoloya. Hata hivyo, kuibuka kwa vyama labda si tatizo, ilimuradi vyama vyote hivi viepuke ushindani na kuzingatia ushirikiano.

Nimewahi kuona hali ambapo vyama vinapanga makongamano yanayosadifiana na kuwatatiza wajumbe wasijue watahudhuria kongamano lipi.

Mara nyingine huku kugonganisha tarehe za makongomano kunaonekana kuwa kwa makusudi kabisa na dalili ya hujuma na suitafahamu kati ya chama kimoja na kingine.

Vyama vyote na vishirikiane na Kamasheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (KAKAMA), asasi iliyoundwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAM) ili kuwezesha usukumaji wa gurudumu la ukuzaji wa Kiswahili.

Kumbuka kauli yangu ya tangu hapo: “Tunajenga nyumba moja, tusigombanie fito!”