Mutyambai anaelekea kuingia afisini kama Inspekta Jenerali mpya

Na CHARLES WASONGA

KAMATI ya pamoja ya bunge la kitaifa na seneti imeidhinisha uteuzi wa Hillary Mutyambai kuwa Inspekta Jenarali mpya wa polisi.

Kwenye ripoti zilizowasilishwa katika bunge la kitaifa Jumanne, Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Usalama na Utawala na ile ya Seneti kuhusu Usalama na Ulinzi zilisema Bw Mutyambai ana ujuzi wa uhitimu wa kumwezesha kutekeleza majukumu ya afisi hiyo.

Kamati hizo zinazoongozwa na Mbunge wa Kiambaa Paul Koinange na Seneta wa Garrisa Yusufu Haji mtawalia, zilisema kuwa Bw Mutyambai alidhihirisha tajriba pana ya kazi za polisi, usalama na uchunguzi kwa miaka 27 ambapo amehudumu katika idara ya polisi.

Hii ni kabla ya kupandishwa cheo hadi kuwa Naibu Mkurugenzi wa idara inayosimamia mapambano dhidi ya ugaidi katika Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS).

Ripoti hiyo ilijadiliwa na kupitishwa Jumanne katika bunge la seneti. Na itajadiliwa katika bunge la kitaifa Jumatano alasiri ambapo pia inatarajiwa kupitishwa kabla ya wabunge kwenda likizo fupi ya siku 10 kuanzia Alhamisi.

Wabunge walitarajiwa kwenda likizo wiki jana lakini Spika Justin Muturi akaiahirisha ili kutoa nafasi kwa wao kujadili ripoti hiyo pamoja na Hotuba ya Rais kuhusu Hali ya Taifa ambayo itatolewa Alhamisi.

Bw Mutyambai anatarajiwa kuchukua nafasi ya Inspekta Jenerali Joseph Boinnet anayeondoka na ambaye majuzi ameteuliwa na Rais Uhuru Kenyatta kuwa Naibu Waziri (CAS) wa Utalii na Huduma za Wanyamapori.