Michezo

Kariobangi Sharks kuonana na Zoo huku Ingwe ikiikabili Chemelil

April 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

UWANJA wa Kenyatta mjini Machakos utakuwa leo Alhamisi mwenyeji wa michuano mitatu ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL).

Mabingwa watetezi wa SportPesa Shield na washikilizi wa SportPesa Super Cup, Kariobangi Sharks wanachuana na Zoo Kericho kuanzia saa tano asubuhi.

Kukamilika kwa mechi hiyo kutapisha mchuano mwingine utakaowakutanisha Vihiga United na wafalme wa 2009, Sofapaka. Kivumbi hicho kitang’oa nanga saa nane alasiri.

Baadaye, Chemelil Sugar watashuka dimbani kumenyana na mabingwa mara 13 wa KPL AFC Leopards ambao kwa sasa wananolewa na kocha mzaliwa wa Rwanda, Casa Mbungo.

Leopards ambao wamekuwa wakisuasua pakubwa katika kampeni za msimu huu, watakuwa na fursa ya kujinyanyua dhidi ya Chemelil ambao wanajivunia hamasa tele.

Chemelil watajibwaga ugani wakijivunia kuwasajili ushindi wa 2-1 dhidi ya mabingwa mara 11 Tusker FC mwishoni mwa wiki jana.

Kufikia sasa, Chemelil wanashikilia nafasi ya 13 kwa alama 21, moja zaidi kuliko Leopards.

Ushindi kwa vijana wa Mbungo utawapaisha hadi nafasi ya 12 na hivyo kuweka hai matumaini ya kutinga mduara wa nane-bora mwishoni mwa kampeni za muhula huu.

Nambari ya 11

Kwa upande wa Chemelil, alama tatu zitawavusha hadi nafasi ya 11 na kuwaruka KCB ambao jana walikuwa wenyeji wa wafalme wa 2008 Mathare United.

Katika mchuano mwingine wa Alhamisi, Nzoia Sugar waliokomolewa na Gor Mahia 2-1 mnamo Jumatatu, watakuwa wenyeji wa Posta Rangers uwanjani Sudi, Bungoma.

Nzoia kwa sasa wanashikilia nafasi ya 12 kwa alama 21, tano zaidi kuliko Rangers ambao wananing’inia padogo mkiani mwa jedwali.

Zaidi ya Zoo Kericho na Mount Kenya United, Rangers pia ni miongoni mwa vikosi ambavyo huenda vikateremshwa daraja mwishoni mwa kampeni za muhula huu.