• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:10 AM
AKILIMALI: Umuhimu wa kujisagia na kuunda chakula cha ng’ombe kuinua uzalishaji wa maziwa

AKILIMALI: Umuhimu wa kujisagia na kuunda chakula cha ng’ombe kuinua uzalishaji wa maziwa

Na SAMMY WAWERU

NG’OMBE ni mnyama wa nyumbani anayefugwa kwa minajili ya ngozi, nyama na maziwa, yakiwa ndiyo mazao makuu.

Ili kuongeza kiwango cha maziwa yanayozalishwa, wanyama hawa wanapaswa kulishwa mlo kamili, ‘balanced diet’. Wafugaji wasiotilia maanani hili wamekadiria hasara kubwa, ng’ombe kula kwa wingi ila mazao ni kiduchu.

Serikali imekuwa ikishauri wakulima kuzingatia mfumo wa kisasa katika ufugaji, suala la lishe iliyoimarishwa ikiwa mojawapo. Wanaoafikia vigezo vya mlo kamilifu, wanaendelea kupiga hatua mbele.

Ili uzalishaji wa maziwa uwe wa kuridhisha, mkusanyiko wa vyakula mbalimbali hasa vyenye ukwasi wa virutubisho vya kutosha kwa ng’ombe unahitajika.

Amos Njane Kamenyi kutoka Thima Coffee Machinery, akionesha nyasi zinavyosagwa kwa kutumia mashine. Picha/ Sammy Waweru

Maziwa yamesheheni Protini, na wataalamu wanapendekeza mlo wake uwe na zaidi ya asilimia 35 ya Protini. Vitamini, Wanga na Mafuta pia ni muhimu.

Madini mengine ya kutilia mkazo katika chakula cha mifugo ni Calcium, Chlorine, Magnesium, Phosphorus, Sodium na Potassium.

“Mkusanyiko huu wa madini ukizingatiwa ng’ombe wataongeza kiwango cha maziwa, mbali na kuimarisha siha,” anasema James Kimemia, afisa wa kilimo na ufugaji Murang’a.

Baadhi ya kampuni za kuunda chakula hiki zimekuwa zikinyooshewa kidole cha lawama, kwa kutengeneza kisichoafikia mkusanyiko wa madini.

Mifuko ya kupakia huorodhesha madini yote lakini mengine hayajajumuishwa, jambo ambalo linalemaza juhudi za wafugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Wakulima wanahimizwa kujitengenezea lishe wao wenyewe, ili kuepuka vikwazo hivyo. Hii ina maana wanahitaji mashine za kuendesha shughuli hii.

Thima Coffee Machinery iliyoko Thika, ni miongoni mwa kampuni zinazouza mashine hizi.

Ina mashine kama Chaff Cutter, Maize peeling & threshing, Rice mill machine, Hydra Chaff Cutter, Silage Machine, miongoni mwa zingine.

Pia, wana mashine za kuchanganya. Amos Njane Kamenyi, mhudumu katika Thima Coffee Machinery, anasema wateja wao wamekadiria mabadiliko makubwa baada ya kujisagia chakula.

“Nyingi ya chakula cha mifugo kinachouzwa madukani, hakijaafikia ubora. Tumepokea habari za kuridhisha wanapojiundia mlo ng’ombe wanaongeza mazao hasa maziwa,” aeleza Bw Njane.

Hasara

Agnes Omingo, mfugaji wa ng’ombe wa maziwa Ongata Rongai, Kajiado, anasema awali alikadiria hasara chungu nzima kupitia chakula cha maduka kabla kubadilisha mkondo huo.

Ng’ombe wala. Picha/ Sammy Waweru

“Niligharamika kununua chakula, ilhali maziwa niliyopokea hayakunipa mapato. Utafiti niliofanya kwa wafugaji waliofanikisha ng’ombe wa maziwa na wataalamu, ulinishawishi kujiundia chakula changu na nimeona mabadiliko makubwa kimapato,” asimulia Bi Agnes. Mfugaji huyu ana mashine aina ya Chaff Cutter, ya Silage, na ya kusaga mahindi.

Nyasi, Napier, mahindi, Boma Rhodes, mihindi, hay, mipunga, Lucerne ni baadhi ya chakula kinachopaswa kusagwa, kisha kuwekwa madini. Ni muhimu kukumbusha mkulima kuwa mifugo wanapaswa kulishwa nyasi zilizokauka, kwani hazina athari kama kuwepo kwa wadudu. Bw Kimemia, mtaalamu wa kilimo na ufugaji, pia anasema nyasi zilizokauka huwapa ng’ombe motisha kunywa maji kwa wingi. “Maji ni kiungo sana kwa ng’ombe kwa kuwa husaidia katika uundaji wa maziwa,” asema mdau huyu.

Bw Njane kutoka Thima Coffee Machinery, anasema mashine wanazouza zinagharimu kati ya Sh20, 000 hadi Sh90, 000.

You can share this post!

AKILIMALI: Mapungufu ya mwilini hayajamzuia kuibuka stadi...

Lionesses yang’ata Uganda, Hong Kong na Papua New...

adminleo