Michezo

Lionesses yang'ata Uganda, Hong Kong na Papua New Guinea

April 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KENYA Lionesses imeonyesha ukatili wake kwa kung’ata Uganda 24-0, Hong Kong 36-5 na Papua New Guinea 20-10 katika mchujo wa raga ya wachezaji saba kila upande wa wanawake ulioanza Hong Kong, Alhamisi.

Mabingwa hawa wa Bara Afrika sasa watakutana na Argentina katika robo-fainali Ijumaa saa kumi na moja asubuhi.

Wakilemea Argentina watakutana na mshindi kati ya Brazil na Kazakhstah katika nusu-fainali.

Katika mechi ya kwanza ya Kundi B, Vipusa wa kocha Kevin Wambua walipepeta majirani Uganda, ambao ni mahasimu wao wakubwa, kwa alama 24-0.

Vipusa wa Kevin Wambua walizamisha Uganda kupitia miguso ya Philadelphia Olando, Janet Okelo, Christabel Lindo na Grace Okulu, ambaye pia alipachika mikwaju miwili.

Lionesses ilirejea uwanjani kwa mechi yake ya pili ikiwa na motisha hata zaidi ya kupata matokeo mazuri na kunyamazisha wenyeji 36-5.

Kuchangia miguso

Okulu na Diana Awino walichangia miguso miwili katika mchuano huu nao Camilla Atieno na nahodha Olando wakapachika mguso mmoja kila mmoja katika mechi hii, ambayo Okulu aliongeza mikwaju miwili naye Janet Owino akafunga mkwaju mmoja.

Sarah Lucas alifunga mguso wa Hong Kong kujiliwaza.

Wakenya walikamilisha mechi za makundi bila kupoteza pale walipopepeta wanavisiwa wa Papua New Guinea kupitia miguso ya Okelo (miwili) na Sheilla Chajira na Awino (mmoja kila mmoja).

Joana Lagona na Debbie Kaore walifungia Papua New Guinea miguso bila mikwaju.

Kenya haijawahi kuwa mshiriki wa duru zote za Raga ya Dunia ya Wanawake, ingawa ilialikwa duru ya Clermont nchini Ufaransa mwaka 2016 na Dubai mwaka 2018. Ikishinda mchujo huu, itashiriki duru zote nane za msimu 2019-2020.