Serikali igharamie safari ya Miguna Miguna kurudi nchini, mahakama yaamuru
Na RICHARD MUNGUTI
Kwa ufupi:
- Jaji Mwita aikashifu serikali kwa kukandamiza haki za wananchi na za Dkt Miguna kwa madai “usalama wa nchi uko hatarini bila kutoa ushahidi”
- Agizo la kuharamisha vuguvugu la National Resistant Movement (NRM) pia lilifutwa
- Miguna naweza kutumia paspoti ya Canada kurudi nchini iwapo idara ya uhamiaji itachelewa kumpa pasi ya KenyaK
- Kurudi nchini kwa Dkt Miguna kufadhiliwe na serikali iliyomtangaza kwa pupa kuwa mhamiaji haramu
KATIKA uamuzi wa kihistoria Mahakama kuu Jumatatu iliamuru mwanaharakati Dkt Miguna Miguna arudi nchini akitumia pasi ya kusafiria ya nchi ya Canada.
Jaji Enock Chacha Mwita aliikosoa serikali kwa kukaidi haki za Dkt Miguna ilipomtangaza kuwa “mhamiaji haramu ilhali ni mzaliwa wa Kenya.”
Jaji Mwita aliikashifu serikali kwa kukandamiza haki za wananchi na za Dkt Miguna kwa madai “usalama wa nchi uko hatarini bila kutoa ushahidi.”
Na wakati huo huo, agizo la kuharamisha vuguvugu la National Resistant Movement (NRM) na Waziri wa Usalama Dkt Fred Matiang’i lilitupiliwa mbali.
Sasa NRM inaweza kuendelea na shughuli zake.
Kabla ya kufurushwa kutoka nchini Dkt Miguna alikuwa “amejitangaza Jenerali wa NRM.”
Arudishwe na serikali
Jaji Mwita aliamuru kurudi nchini kwa Dkt Miguna kufadhiliwe na serikali iliyomtangaza kwa pupa kuwa “mhamiaji haramu ilhali ni mzaliwa wa eneo la Nyando katika Kaunti ya Kisumu na aliwania kiti cha Ugavana Nairobi na kushindwa na Bw Mike Sonko Mbuvi.”
Aidha, alilitaka shirika la kitaifa la kutetea haki za binadamu nchini (KNHRC) lihakikishe Dkt Miguna hasumbuliwi akiwarudi nchini.
Jaji huyo aliharamisha maamuzi yote ya Dkt Matiang’i na Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji Gordon Kihalangwa ya kumtangaza Dkt Miguna kuwa mhamiaji haramu.
Pia alifutilia mbali uamuzi wa Mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji wa kutotambua cheti cha usafiri cha Dkt Miguna alichopata akiwa nchini Canada.
Atumie paspoti ya Canada
“Mlalamishi anaweza kutumia paspoti ya Canada kurudi nchini iwapo idara ya uhamiaji itachelewa kumpa pasi ya Kenya.”
Aliongeza kusema kuwa asasi zote za serikali zinapasa kuimarisha utekelezaji wa Katiba. Kila mmoja nchini Kenya anatakiwa kuhakikisha kwamba Katiba iliyo sheria kuu nchini imefuatwa na haki za wananchi hazikandamizwi.
Mahakama iliwashutumu maafisa wakuu Serikalini waliokiuka Katiba na sheria na kumfurusha Dkt Miguna Miguna kutoka nchini “akisubiriwa mahakamani na Jaji Luka Kimaru.”
Jaji Mwita alisema Dkt Miguna amewasilisha kesi iliyo na mashiko makuu kisheria na kwamba haki zake zilikandamizwa.
“Ushahidi katika kesi unahitaji kutolewa na mlalamishi mwenyewe kisha ahojiwe na wakili wa Serikali Bw Emmanuel Mbittah,” alisema Jaji Mwita.