Michezo

Kenya yaangamiza Tunisia raga ya Afrika U-20

April 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

KWA mara ya sita katika makala saba ya Raga ya Afrika ya wachezaji 15 kila upande ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 itakutanisha Kenya na Namibia baada ya wenyeji Chipu kuaibisha Tunisia 73-0 katika nusu-fainali ya pili ya Kundi A ya Barthes Trophy jijini Nairobi, Alhamisi.

Kenya, ambayo timu yake ya Chipu ilikanyagwa na Namibia katika fainali za mwaka 2013, 2014, 2016, 2017 na 2018, imejikatia tiketi ya kushindai taji kupitia miguso 11 iliofunga kupitia kwa Beldad Ogeto (minne), Geoffrey Okwach na George Maranga (miwili kila mmoja) nao Bonface Ochieng’, Michele Brighetti, Barry Young na George Kiryazi wakachangia mguso mmoja kila mmoja.

Dominic Coulson, ambaye hana klabu, alichangia alama 18 kutokana na mikwaju tisa. Mabingwa watetezi Namibia walishinda Senegal 45-12 katika nusu-fainali ya kwanza.

Mshindi kati ya Kenya na Namibia hapo Aprili 7 atajikatia tiketi ya kuenda Brazil kwa mashindano ya dunia ya Junior World Rugby Trophy (JWRT) yatakayofanyika Julai 9-21.

Senegal na Tunisia zitamenyana katika mechi ya kutafuta nambari tatu ambapo mshindi atasalia katika mashindano haya ya daraja ya juu ya Afrika. Atakayepoteza kati ya Senegal na Tunisia atashushwa ngazi hadi Kundi B.