ANA KWA ANA: Ni kweli, ‘The Trend’ imejenga brandi yangu
Safu hii ilikutana naye akiwa kwenye harakati zake za kupanga kazi na kupiga naye stori hivi:
Hivi kwa asiyekufahamu, Butita ni nani?
Butita: (Akicheka) Hivi kuna asiyenifahamu kweli? Pengine majuu. Ila tuachane na utani. Mimi ni chale kama ninavyofahamika na wengi, lakini pia mimi ni mbunifu na msanifu wa vichekesho, Emcee na vilevile produsa wa vipindi vya ucheshi.
Ulijikutaje kwenye sanaa hii?
Butita: Mwanzo ucheshi naamini ni kipaji lazima uwe umejaliwa nacho. Ila kwa kuwa umetaja sanaa, nilianza kama mwimbaji (hehehe). Muziki niliokuwa najaribu kuufanya ulikuwa wa vichekesho hivi. Nilirekodirekodi kwenye vistudio vya kimtaa. Ila nakumbuka kipindi fulani nilikwenda Calif Records iliyokuwa ikivuma wakati huo ili nirekodi na produsa Clemmo. Kufika nilikuta foleni ndefu na ikawa ndiyo mwisho wa muziki wangu.
Hapo ndipo ukaamua ufanye komedi?
Butita: Toka mwanzo, kitu nilichokuwa natamani kufanya ni komedi. Ila wakati naanza, aina ya komedi niliyokuwa nikiifahamu ni ile iliyokuwa ikifanywa na marehemu Mzee Ojwang, Mama Kayai kupitia vile vipindi vya Vitimbi, na Vioja Mahakamani. Sikuwa najua ni wapi pa kuanzia ila kipaji kilikuwa kikiniwasha. Ni kwenye harakati hizo ndipo ikatokea Churchill Show.
Endelea…
Butita: Churchill Show ilipoanza, ilikuja na aina mpya ya komedi ‘Stand Up Comedy’ ambayo wengi wetu hatukuwa tunaifahamu.
Sasa nilisikia kuna auditions zinafanyika, nikaamua kwenda kujaribu bahati yangu na kwa hakika nilipoangusha mistari baada ya kupewa maelekezo ya ninachotakiwa kufanya, maprodusa wakanogewa. Hapo nikajiunga na Churchill Show rasmi Desemba 2010 na kwenda laivu mara ya kwanza 2011.
Churchill Show ilikujenga ila ni kama baadaye uliondoka?
Butita: Ndio sipo kwa sana vile kama hapo nyuma, ila siwezi kusema niliondoka. Hii ni kwa sababu tumekuwa na uhusiano wa muda mrefu wa kikazi na bado tunashirikiana nao ila sina mkataba nao.
Hivi wajua kando na mimi kuwa mcheshi wa Churchill Show, pia walinipa kazi ya kuwa mkuu wa ubunifu na usanifu vichekesho pale? Mara nyingi vichekesho vya wasanii waliopanda stejini, vilipitia kwangu mwanzo, nikavihakiki na hata kuviongeza nguvu palipostahili, kabla ya kuwasilishwa kwa hadhira. Kazi hii niliifanya hadi 2016 nilipojiunga na The Trend.
Kwa hiyo ‘The Trend’ ndiyo ilikung’oa Churchill Show?
Butita: Wajua Churchill Show huja ikisita. Sasa wakati ilisita 2011 nikawa sina kazi ya kufanya. Wakati nikiwa kwenye harakati ya kutafuta cha kufanya nikiwa nimejiunga tu na Kona Comedy 2012, mtangazaji Larry Madowo wakati huo akiwa anafanya kazi Nation, alimwalika rafiki yangu kuja kwenye mahojiano kwenye Nation FM. Nikaamua kumsindikiza, ila shoo ilipoanza, Madowo alinogewa na tukaishia kuifanya sote watatu. Baada ya hapo ndipo alihisi anaweza kuniongeza kwenye shoo ya The Trend. Hivyo ndivyo kitengo cha TTTT- The Trending Topic Talkers kilivyozaliwa na nikawa mdau mpaka leo.
Unaonekana umeridhika zaidi kuwa kwenye The Trend zaidi ya Churchill Show?
Butita: Wakati nikihisi nina mistari huwa natokea kwenye Churchill. Ila ieleweke kuwa The Trend ni fursa tofauti kabisa. Imeweza kunifanya kuonyesha uwezo wangu mwingi tofauti na Stand Up Comedy. Pia imenisaidia kuikuza brandi yangu hata zaidi.
Wewe ni mtu maarufu na kwa kawaida skendo huwaandama?
Butita: Hehehe! Naona unavyokuja.
Umevumishwa kuwa kwenye uhusiano na mcheshi mwenzako Mammito, hili ni kweli?
Butita: Haya nafikiri ni maisha ya kibinfasi. Pamoja na ustaa nina pia maisha ya kuishi na kwa kuwa mimi ni mtu msiri sana na maisha yangu, naomba jibu lako nilisukume chini ya zulia kidogo.
Uhusiano wako na Mammito upoje?
Butita: Duh! Mbona umekwamia pale. Sisi ni wasanii kwenye tasnia moja.
Kwa hiyo nikisema nyie ni marafiki sitakosea?
Butita: Nina uhusiano mzuri na wacheshi wote wa kike hapa nchini.
Nayo ishu kwamba Mammito alinasa ujauzito wako?
Butita: Hili swali nafikiri linamfaa yeye zaidi.