Makala

DOMO KAYA: Mbosso mshikaji wangu, kweli ungekuwa wakili tu

April 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANAMIPASHO

PENGINE mshikaji wangu Mbosso kutoka WCB, yupo kwenye taaluma isiyomfaaa kabisa. Amenifanya kuamini kwamba, kama leo angelikuwa wakili, basi angeshinda kesi zote mbele yake, hata itokee akamwakilisha muuaji wa kukusudia.

Nimemshuhudia Mbosso akikana peupe maneno yake mwenyewe, tena kwa kuvalia sura ngumu, kaitafuna kabisa kauli yake iliyozua utata mkubwa.

Wikendi iliyopita, Mbosso Khan alipanda kwenye Instagramu yake na kuposti mjengo wa nguvu wa vyumba vitatu kisha kuachia posti ndefu, ambayo pindi unapomaliza kuisoma, inakusadikisha kuwa kanunua mjengo huo.

Thamani ya mjengo huo anaosema kwa sasa anaumiliki inakadiriwa kuwa Tsh90 milioni, ambazo ni sawa na Ksh4 milioni.

Kwenye posti yake, Mbosso amewashukuru sana mashabiki wake kwa kumfikisha alipo kwa sasa toka alipoamua kuwa msanii solo baada ya bendi yao ya Yamoto kusambaratika.

WCB walimchukua na kwa hakika Mbosso amekuwa akijituma sana. Ana hiti nyingi kwa sasa zaidi ya hata alizofanikisha kutoa akiwa na Yamoto.

Kwa maana hiyo ni kwamba, mafanikio ya muziki wake pia, ni mafanikio kwenye suala la kuingiza mkwanja.

Ndani ya mwaka mmoja toka awe solo, Mbosso alidai kumiliki mjengo wa Ksh4 milioni. Sio kwa kasi hiyo. Nasema hivi kwa nini?

Mwanzo kabisa, Mbosso kasainiwa na WCB ambayo chanzo cha karibu kimeniarifu kuwa mkataba wake pale nao ni wa miaka 15.

Halafu tena, mkataba huo umechorwa kwa namna ambavyo asilimia kubwa ya pato analoingiza linakwenda kwa lebo, na anachobakia nacho, pengine atahitaji kuchanga kwa miaka zaidi ili kuja kufanya kitu cha maana.

Huu ndiyo ukweli unaofichwa na WCB ambayo mimi nimeibiwa siri na mdau mmoja aliyewahi kufanya kazi pale.

Na kama unadhania ni chuki, basi mwangalie Harmonize.

Ni mangapi makubwa kafanya zaidi ya kuwa mkali wa pamba? Hata mjengo wa mamake aliomjengea, kwa hadhi aliyojipaisha, nilitarajia ungetisha zaidi.

Menejimenti hiyo

Ndiyo maana ilikuwa vigumu sana kwangu kuamini kuwa Mbosso kanunua mjengo wa bei hiyo tena kwa haraka hivyo. Baada ya chakurachakura zangu, nilibaini kuwa ni menejimenti yake imemkodishia mjengo huo wa kifahari.

Pia dalali wa mjengo huo alifichuliwa na kuonyesha mjengo kaukodisha kwa Ksh52,000 kila mwezi.

Lakini kwenye posti yake ndefu nikinukuu sentensi moja hivi, Mbosso kasema “…Hiki ni kidogo mlichoweza kunifanya nimiliki leo kijana wenu” Kauli ambayo kailenga kwa mashabiki wake.

Katikati mwa juma, Mbosso kahojiwa kuhusu utata huo, na karuka stori kwa kusema hakuna sehemu aliyoandika kuwa kanunua nyumba. Hapo ndiyo mwanzo kanipoteza.

Hivi maana ya kumiliki kitu ni nini? Ndio hakuandika kanunua mjengo ila alisema anaumiliki mjengo huo. Hii ina maana gani?

Ndiyo maana nilitanguliza kwa kusema hivi, Mbosso anaweza kuwa wakili moja hatari sana.

Kwa staili hii ya kuwahadaa mashabiki wake kwa jinsi anavyopindisha maneno, basi kapita na gredi ya A.

Ndiyo usanii huu, wakati mwingine lazima ufeki maisha yasiyo yako. Au ndio kwa misingi ya kiki? Lakini pataharibika nini kwa kuwa mkweli tu kama alivyo Akothee?