Kenya Lionesses yazimwa na Brazil
Na GEOFFREY ANENE
MATUMAINI ya Kenya kuwa na timu mbili kwenye Raga ya Dunia yamezimwa baada ya Lionesses kuzidiwa ujanja na Brazl katika nusu-fainali kwa alama 17-5 mjini Hong Kong mnamo Ijumaa katika mechi za kufuzu kushiriki Raga ya Dunia ya Wanawake ya msimu 2019-2020.
Lionesses, ambayo ilizimwa na Afrika Kusini katika nusu-fainali ya mchujo wa mwaka 2018 mjini Hong Kong, iliingia mechi ya Brazil ikiwa na motisha ya kupepeta Uganda (24-0), Hong Kong (36-5) na Papua New Guinea (20-10) katika mechi za kundi B na kuzaba Argentina 17-15 katika robo-fainali.
Hata hivyo, vipusa wa Kevin Wambua walijipata mashakani mapema baada ya Bianca Dos Santos Silva kuweka Brazil kifua mbele kupitia mguso dakika ya pili.
Mabingwa wa Afrika, Kenya, walijikakamua na kusawazisha 5-5 kupitia Janet Okelo dakika tatu baadaye baada ya mtimkaji huyu kutumia vyema mguu wake wa kulia kupiga mpira na kisha kuukimbiza na kufunga mguso.
Hata hivyo, kwa kutumia pasi safi na kunyima Kenya mipira, Brazil ilichukua uongozi tena 10-5 kupitia kwa mguso wa Bianca Dos Santos Silva.
Kenya iliponea kujipata chini zaidi wakati wa mapumziko baada ya kufungwa mguso mwingine, lakini refa Ashleigh Murray akaukataa kwa sababu Brazil ilikuwa imerombeza.
Hata hivyo, mtupo mbaya kutoka kwa Wakenya karibu na kisanduku chao cha miguso uliipa Brazil nafasi nzuri ya kuimarisha uongozi wao hadi 15-5 kupitia kwa Luiza Gonzalez Da Costa Campos, huku Raquel Kocchann akiongeza mkwaju.
Ilikuwa wazi Kenya haikuwa katika mechi hii kwani iliadhibiwa zaidi ya mara tano dhidi ya moja kwa upande wa Brazil, ambayo pia ilitawala umegaji wa pasi kwa pasi 48-8.
Lionesses pia ilifika nusu-fainali ya mwaka 2018 ikichapwa na Afrika Kusini 12-7.
China ilishinda mchujo wa mwaka 2018 na kujikatia tiketi ya kushiriki duru zote za Raga ya Dunia ya wanawake msimu 2018-2019.
Mwaka 2019, fainali itakutanisha Brazil na Scotland, ambayo imecharaza Japan 24-19 katika nusu-fainali ya pili.
Attachments area