UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Lugha kama bidhaa na aina mbalimbali za lugha
Na MARY WANGARI
JE, lugha inaweza kuwa bidhaa?
Ni muhimu kufahamu kwamba Kiswahili ni bidhaa kama tu bidhaa nyinginezo na kinaweza kuuzwa na kununuliwa sokoni.
Aghalabu, mchakato wa kubidhaisha Kiswahili unajitokeza wakati ambapo wenyeji au wazawa wa lugha ya Kiswahili wanatoa mafunzo ya lugha ya Kiswahili kwa watu ambao lugha hii sio mame lugha yao.
Madhumuni hasa ya kufundisha Kiswahili kwa wageni ni pamoja na:
- Kumpa mwanafunzi uwezo wa kuimudu lugha vizuri
- Kumpa mwanafunzi uwezo wa kuwasiliana na wazawa wa lugha husika
Kabla ya kujitosa katika tasnia ya ufundishaji wa lugha ya Kiswahili kwa wageni ni muhimu kujifahamisha kwa kina kuhusu dhana ya lugha pamoja na aina mbalimbali za lugha jinsi ifuatavyo:
Dhana ya lugha
Jinsi tunavyofahamu, lugha ni mpangilio wa sauti na maneno unaoleta maana na ambao hutumiwa na watu wa taifa au kundi fulani kwa ajili ya kuwasiliana.
Kuna aina mbalimbali za lugha kulingana na matumizi yake jinsi ifuatavyo:
Lugha mama
Hii ni lugha ambayo mwanajamii hujifunza kutoka kwa wazazi wake, jamaa au majirani.
Lugha ya kwanza / lugha tangulizi
Hii ni lugha anayojifunza mtu maishani anapoanza kuzungumza.
Lugha kienzo
Hii ni lugha au mfumo fulani wa ishara ambao hutumiwa kufafanulia au kuendelezea lugha nyingine.
Lugha mame
Ni lugha ambayo bado imo katika umbo lake la awali. Aghalabu, lugha hiyo ndiyo ambayo huwa imezizaa lugha nyinginezo.
Lugha azali
Hii ni lugha ambayo huzaa lugha nyingine. Lugha zinaweza kuzaliwa na moja lakini baadaye zikaanza kutofautiana kidogo, hatimaye zikawa lugha tofauti.
Lugha nasaba
Hizi ni lugha ambazo chimbuko lake ni moja. Kwa mfano, lugha zote za Kibantu ni lugha nasaba kwa kuwa zinatokana na asili moja Bantu mame.
Lugha rasimi
Ni mtindo wa lugha wa kizamani ambao ulitumiwa na watu fulani maarufu na ukaaminika kuwa ni mtindo bora wa lugha unaofaa kuigwa na watu wengine. Kwa mfano, Kiingereza kilichotumiwa na William Shakespeare katika tamthilia zake.
Marejeo
Tumbo Masobo, Z.N., Chiduo, F.K.F. (2007). Kiswahili Katika Elimu. Dar es Salaam; Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (TUKI).
Mogambi, H., (2008). KCSE Golden Tips Kiswahili. Nairobi: Macmillan Kenya.
Ipara, I. O., & Maina, G. (2008). Fani ya Isimujamii kwa Shule za Sekondari. Nairobi: Oxford University Press.