UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sifa bainifu za lugha ya taifa
Na MARY WANGARI
SIFA za lugha ya taifa
- Inapaswa kuwa inayovuka mipaka ya kabila fulani ili isiwe lugha ya kikabila.
- Inafaa kuwa lingua franca katika taifa fulani. Inapokuwa lingua franca, inakuwa inazungumzwa na watu wa makabila mbalimbali na wala sio kabila moja pekee.
- Inapaswa kuwa lugha ya mama ya kikundi fulani cha watu katika taifa husika. Sifa hii ina umuhimu kwa kuwa huwezesha kuwakilisha utamaduni wa wenyeji na kuwachochea wengine kujifunza lugha hiyo.
- Wazungumzaji asilia wa lugha hiyo wanakuwa kama kielelezo na walimu wa kueneza lugha hiyo
- Inapaswa iwe na muundo wa kiisimu unaofanana na baadhi ya lugha mame za jamii husika. Sifa hii inafanya ufundishaji wa lugha hii kuwa rahisi.
- Inapaswa kuwa lugha mojawapo ya kienyeji zinazozungumzwa katika taifa fulani, yaani lugha ya taifa isiwe lugha ya kigeni katika taifa husika. Hii ni kwa sababu lugha ya kienyeji inasheheni chembechembe muhimu za utamaduni wa wenyeji ambazo hazifai kupotoshwa katika lugha za kigeni.
- Hueneza hisia za kizalendo na utaifa.
- Huunganisha watu hivyo huondoa chuki
Lugha ya taifa ina majukumu yafuatayo:
- Ni kifaa cha kuziba mipaka ya kikabila.
- Ni nyenzo ya kuwaunganisha watu wenye asili mbalimbali na kuwafanya kuwa kitu kimoja.
- Ni ishara ya umoja wa kitaifa.
- Husaidia kufanikisha harakati za uongozi kutokana na kuhimiz amatumizi ya lugha moja ambayo inarahisisha jukumu la serikali katika uongozi.
- Huleta maendeleo ya kijamii, kisiasa, kiuchumi na kisayansi.
- Hutambulisha watu wa taifa fulani na kuleta hisia za kizalendo miongoni mwao.
- Ni ala inayolipa taifa na wananchi wake hadhi na haiba. Kwa mfano, Kiswahili kama lugha ya taifa nchini Kenya na Tanzania huyapa mataifa hadhi na kuwapa taswira ya watu wenye upekee wao wa taifa na pia asili yao ya Kiafrika.
- Huweza kuwa ua wa kutenganisha wananchi kwa kuwa huweza kuweka mipaka baina ya wale wanaoitumia na wale wasioitumia.
- Hutoa nafasi ya ajira kwa wasomi wake.
- Inakuza mifumo ya mawazo na mielekeo inayojenga utamaduni mwafaka wa kitaifa.
Marejeo
Chiraghdin, S., Mnyampala, M. (1977). Historia ya Kiswahili. Nairobi: Oxford University Press.
Richards, J.C. (1984). Error Analysis Perspectives on Second Language Acquisition. London: Longman Group Ltd.
Wardhaugh, R. (1986). An Introduction to Socio-Linguistics. New York: Blackwell Publishers.